Mapasta 200 walinajisi zaidi ya watu 700 – Ripoti
MASHIRIKA Na PETER MBURU
ZAIDI ya maafisa 200 wa kanisa la Southern Baptist la Amerika na watu wengine wa kujitolea wamepatikana na hatia ya dhuluma za kingono kwa miongo miwili iliyopita, ripoti imesema.
Waendesha injili, mapasta, wafanyakazi wa kujitolea, madikoni na walimu wa watoto ni baadhi ya watu waliotajwa na jarida la Houston Chronicle kama walioshiriki dhuluma za kingono, katika uchunguzi wa kina kuhusu sakata ya dhuluma za ngono ndani ya kanisa hilo.
Takriban viongozi 250 wa kanisa na wafanyakazi wa kujitolea kwa hiari wameshtakiwa, japo kwa jumla watu 380 wametuhumiwa kujihusisha na maovu hayo tangu 1998.
Inadaiwa kuwa kuna takriban wadhulumiwa 700, huku baadhi yao wakiwa watoto wa hadi umri wa miaka mitatu, uchunguzi huo wa mwaka mzima ukabaini.
“Wengi wa wadhulumiwa walikuwa vijana matineja ambao walitumiwa picha na jumbe chafu, kuonyeshwa kanda za ngono na kupigwa picha wakiwa uchi, ama mara kwa mara wakanajisiwa na mapasta vijana,” ripoti hiyo ikasema.
“Baadhi ya wadhulumiwa wa hadi umri wa miaka mitatu aidha walidhulumiwa ama kunajisiwa ndani ya afisi za mapasta ama vyumba vya mafunzo ya watoto kanisani,” ripoti hiyo ikatoboa.
Wasimamizi wa kanisa wanadaiwa kukosa kufahamisha serikali kuhusu malalamishi kuhusu visa hivyo katika baadhi ya matukio, ripoti hiyo ikasema.
Baada ya ufichuzi huo, watu wamekashifu kanisa hilo la Sothern Baptist, wakitaja maovu hayo kuwa ushetani.
Kanisa hilo lina matawi takriban 47,000 na baada ya ripoti hiyo na ghadhabu za umma lilijitokeza kulaani washukiwa na kusimama na wadhulumiwa.
“Tunawataka watu wote waliochangia na kuwezesha dhuluma kutubu na kukiri thambi zao kwa Yesu Kristo na wasimamizi wa kanisa na kwa serikali,” likasema.