Makala

Kukuza imani ya mtoto enzi hizi za dijitali

Na BENSON MATHEKA September 7th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

Katika enzi hii ya kidijitali, malezi yameingia katika eneo lisilojulikana. Mitandao ya kijamii, mawasiliano yasiyokoma, na shinikizo la kuonekana kuwa bora vimeongeza changamoto katika kulea watoto walio na afya ya kihisia.

Wazazi wengi hutamani kukuza hali ya kujiamini kwa watoto wao, lakini tabia fulani za kisasa huenda zikawa kizingiti bila wao hata kugundua.

Wazazi mara nyingi huweka picha au mafanikio ya watoto wao mtandaoni kwa nia njema. Lakini tabia hii inaweza kuwa na athari zisizotarajiwa. Watoto huenda wakajihisi wameanikwa, wakaaibika, au kuhisi shinikizo la kufikia matarajio fulani hatua inayoathiri kujiamini kwao.

Mtoto anapoona mafanikio yake yakitangazwa mtandaoni kila mara, huenda akaanza kufikiria kuwa mafanikio ni sawa na maoni yanayotolewa na wafuasi wa mzazi katika mitandao ya kijamii na kumfanya ajiamini kupita kiasi.

“Kabla ya kuchapisha picha ya mwanao, muulize mtoto wako ruhusa. Heshimu mipaka yake na fikiria jinsi atakavyohisi kuhusu maudhui ya hadharani. Wape nafasi ya kumiliki simulizi yao, usiachie mtandao upange mwelekeo wao,” asema mtaalamu wa malezi dijitali Samuel Kae.

Anasema kwamba kuwalinganisha watoto na wenzao, hata kwa nia nzuri, kunaweza kuwafanya wajihisi hawatoshi. “Kauli kama “Tazama jinsi fulani anavyopiga piano vizuri” huonekana kama kumtia mtoto hamasa, lakini mara nyingi huleta madhara,”asema.

Wataalamu wanahimiza wazazi kukumbuka kuwa kila mtoto hukua kwa mwendo wake. Kuwalinganisha na wengine huongeza shinikizo na wasiwasi usio wa lazima, jambo ambalo linaweza kuwafanya waachane na shughuli walizopenda hapo awali.

Kae anashauri wazazi kushangilia vipaji vya kipekee vya kila mtoto wao. “ Badala ya kulinganisha watoto, zingatia maendeleo ya kila mmoja na kutambua juhudi zao hata zile ndogo,” asema.

Ni rahisi kutumia vifaa vya dijitali kufanya kazi nyingi wakati wa muda wa familia. Hata hivyo, matumizi kupita kiasi – ya mzazi au mtoto – yanaweza kuacha watoto wakihisi kupuuzwa au kutothaminiwa.

Watoto wanapohisi kupuuzwa kwa sababu ya simu au kifaa kingine, huenda wakahisi hawana umuhimu. Hata dakika tano za mazungumzo ya dhati zinaweza kuleta tofauti kubwa katika hisia zao, wakahisi usalama na wenye thamani.

Tengeneza maeneo au nyakati zisizo na teknolojia – kama vile wakati wa chakula cha familia au kabla ya kulala. Tumia muda huo kuwasiliana moja kwa moja na kuonyesha mtoto wako kuwa ni wa thamani kuu kwako.

“Ni kweli malezi katika enzi ya kidijitali yana changamoto zake, lakini pia yana nafasi ya kujenga watoto waliokomaa kihisia na walio na hali thabiti ya kujiamini. Mzazi  akiwa  mwangalifu kuhusu vitendo yake   mtandaoni na nje ya mtandao anaweza kuwasaidia watoto kukuza imani ya kweli ndani yao.