HabariHabari Mseto

ODM yarudisha Kombe Magarini, Moi akitapatapa Baringo

Na NDUBI MOTURI na FLORAH KOECH September 12th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

CHAMA cha Orange Democratic Movement (ODM) kimemteua rasmi aliyekuwa Mbunge wa Magarini, Harrison Kombe, kuwania tena kiti hicho katika uchaguzi mdogo unaotarajiwa kufanyika Novemba 27, 2025.

Uamuzi huu ulitangazwa huku chama hicho kikikabiliwa na presha kubwa ya kuteua wagombeaji katika maeneo mengine yaliyo na ushindani mkali.

Kombe alipata tiketi ya moja kwa moja kutoka ODM baada ya chama kubaini hakuwa na mpinzani wa moja kwa moja.

Hatua hiyo ilijiri miezi michache baada ya Mahakama Kuu kufuta ushindi wake wa mwaka 2022 kutokana na dosari katika mchakato wa uchaguzi.

Kwa sasa, ODM ina matumaini kuwa kwa kumsimamisha Kombe tena, itaweza kurejesha kiti hicho ambacho ni miongoni mwa ngome zake katika Kaunti ya Kilifi.

Wakati huohuo, ODM imetangaza kuwa kutakuwa na mchujo katika maeneobunge ya Ugunja na Kasipul kati ya Septemba 24 hadi Septemba 27, kutokana na mvutano na idadi kubwa ya wagombeaji waliojitokeza kutaka tiketi ya chama.

Kiti cha Ugunja kiliachwa wazi baada ya aliyekuwa Mbunge, Opiyo Wandayi, kuteuliwa kuwa Waziri, huku Kasipul kikibaki wazi kufuatia kifo cha Mbunge Charles Ong’ondo Were.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa ya Uchaguzi ya ODM, Bi Emily Awita, amesema mchujo huo utaendeshwa kwa uwazi na haki, akisisitiza kuwa chama hicho kina nia ya kuendeleza demokrasia ya ndani kwa vitendo.

“Tunataka kuhakikisha kila mwanachama ana nafasi sawa, na kwa maeneo yenye ushindani mkubwa, mchujo ndio njia bora ya kuamua mgombeaji,” alisema Awita.

“ODM ni chama cha watu, na kwa kuwapa fursa ya kuchagua viongozi wao, tunathibitisha kuwa tumejizatiti kuimarisha misingi ya demokrasia si tu ndani ya chama, bali pia katika taifa zima,” aliongeza.

Katika maeneo mengine kama vile Chewani, Kisa Mashariki, Purko, na Namaan, wagombeaji waliopatikana bila mpinzani walipewa tiketi za moja kwa moja.

Huku ODM ikikamilisha maandalizi ya chaguzi ndogo hizo, macho ya taifa pia yameelekezwa Kaunti ya Baringo, ambako aliyekuwa Seneta, Gideon Moi, bado hajatangaza iwapo atagombea tena kiti hicho kilichoachwa wazi baada ya kifo cha Seneta William Cheptumo wa UDA.

Ukimya wa Moi umeibua maswali kuhusu hatima ya kisiasa ya ukoo wa Moi katika siasa za Rift Valley.

Chama cha KANU, ambacho Moi anaongoza, bado hakijatoa msimamo rasmi, ingawa shinikizo kutoka kwa viongozi wa eneo hilo zinaendelea wakimtaka arejee ulingoni. Kwa upande wake, Moi amesema bado anashauriana.

“Kuna mambo mengi mbele yetu. Wakati ukifika, nitarejea kwa wananchi, mkinisindikiza kwa moyo mmoja, basi kila kitu kitaenda sawa,” alisema Moi katika mkutano wa hadhara huko Kabartonjo.

“Siasa hazihitaji haraka, ni subira. Nitasikiliza wananchi wangu kwanza, kisha nitafanya uamuzi wa busara,” aliongeza.