Polisi wapanua uchunguzi kuhusu mauaji ya wakili Mbobu, walenga watu 8
Polisi wamepanua uchunguzi wao kuhusu mauaji ya wakili Kyalo Mbobu, yaliyotokea siku ya Jumanne, kwa kulenga watu wanane kama wahusika wa karibu japo hawajapata mshukiwa.
Mbali na watu watatu ambao walizuiliwa Ijumaa, timu ya kitengo cha Upelelezi wa Jinai (DCI) inatafuta wengine watano. Miongoni mwa walio chini ya uchunguzi ni mtu aliyeonekana akimfuata Mbobu kutoka kwa ofisi yake huko Kaunda Street.
Wachunguzi wanasema mtu huyo alikuwa amevaa koti nyeusi na T-shirt nyeupe. Alionekana kwenye video akipiga simu, lakini akakata Mbobu alipopita karibu naye.
“Tisa hao wanachukuliwa kama watu wa umuhimu. Wachunguzi wanafuata nyendo zao zaidi,” alisema afisa mmoja wa polisi, ambaye hakutaka kutajwa jina.
Mbobu, aliyewahi kuwa mwenyekiti wa Jopo la Kutatua Migogoro ya Vyama vya Kisiasa, alipigwa risasi mara nane akiwa Magadi Road alipokuwa akiendesha gari kurudi nyumbani. Mtu mmoja aliyekuwa kwenye pikipiki alikimbilia upande wa gari la Mbobu na kumpiga risasi.
Afisa mmoja wa DCI aliambia Taifa Leo kuwa polisi wameshaanza kufuatilia vidokezo kuhusu watu hao wanane, wakisema wanaweza kuwa na taarifa muhimu au hata walihusika moja kwa moja katika tukio hilo.
Ijumaa asubuhi, polisi walikamata watu watatu- mwanasiasa, mpwa wake, na mfanyabiashara – na kurekodi taarifa zao katika makao makuu ya Polisi, Nairobi kabla ya kuhamishiwa vituo vingine vya polisi.
Mwanasiasa huyo alipelekwa Kituo cha Polisi Kileleshwa, mpwa wake yuko Kituo cha Polisi Kilimani, na mtu wa tatu alipelekwa Kituo cha Polisi Capitol Hill.
Watu hao watatu ni majirani wa Mbobu mtaani Karen.
Kupitia wakili wake Musa Maulid, mwanasiasa huyo amekana kumjua Mbobu au kufanya biashara pamoja naye. Alisema kuwa alikuwa Sagret Hotel, ambapo watu hao watatu walikutana na Mbobu kwa chakula cha mchana pamoja na mpwa wake, na walikuwa wakabadilishana stakabadhi za mradi ambao haujafahamika.
Mwanasiasa huyo alisema kwamba alikutana na rafiki yake,katika hotel hiyo ya Sagret na walizungumza na Mbobu kwa dakika chache.
Baada ya kusalimiana na Mbobu, alisema alimaliza mkutano na mpwa wake na kuondoka kwenda Yaya Centre kwa masuala mengine ya kazi.
Katika taarifa yake alisema kuwa baada ya kuondoka Kilimani, alitembelea Ndeiya, ambapo ana shamba. Alieleza kuwa alifika hapo takriban saa 9 alasiri na kuondoka kurudi Karen saa moja kwa chakula cha jioni.
Polisi wanasema walipata kiasi kikubwa cha pesa nyumbani kwa mwanasiasa huyo. Kulingana na wakili wake, pesa hizo ni halali.
Mtu wa tatu aliyechukuliwa kama wa umuhimu, mfanyabiashara ambaye alikuwa akifanya mazoezi na Mbobu, amesema kwa wachunguzi kuwa baada ya mkutano katika Sagret, alirudi nyumbani. Alisema kuwa baadaye siku ya Jumanne aliposikia taarifa za kifo cha Mbobu kwenye vyombo vya habari, alienda haraka nyumbani kwa wakili huyo kutoa pole kwa familia.
Uchambuzi wa kisayansi wa simu ya Mbobu, unaoendelea, umeisaidia DCI kuandaa orodha ya watu wanaoshukiwa