Ukraine yanyaka Wakenya wakipigana kwa niaba ya Urusi vitani
WANAJESHI wa Ukraine wanaendelea kuwazuilia zaidi ya Wakenya wanne ambao imebainika walinyakwa wakipigania jeshi la Urusi.
Ukraine na Urusi zimekuwa na mzozo wa zaidi ya miaka mitatu kuhusu mipaka yao na Wakenya hao walikuwa wakipigania Moscow dhidi ya Kyiv.
Afisa mmoja kutoka Ubalozi wa Ukraine Alhamisi alisema Wakenya wanne ni kati ya raia wa mataifa mengine ambayo walishawishiwa kuingia kwenye jeshi la Urusi ili kupigania taifa hilo.
Wakenya hao wanne ni Peter Njenga, Felix Mutahi, Martin Munene na mwanaume ambaye alitambulishwa tu kwa jina Evans.
Video ambayo ilichapishwa kwenye ukurasa wa Facebook mnamo Juni iliwaonyesha Njenga, Mutahi na Munene wakijitambulisha kati ya raia wengine wa kigeni, wakijianda kujiunga na wanajeshi wa Urusi kuvamia Ukraine.
Msemaji wa Serikali Isaac Mwaura na Katibu katika Wizara ya Masuala ya Kigeni Korir Sing’oei hawakuwa wamejibu Taifa Leo kuhusu hatima ya wanajeshi hao wakati wa kuchapisha habari hii.
Bado haijabainika jinsi na mbona Wakenya walijiunga na jeshi la Urusi.
Hata hivyo, hapo awali Taifa Leo imewahi kubaini kuwa raia wengi kutoka Bara la Afrika wamekuwa wakifurika Urusi ili kujiunga na jeshi lake katika mapambano dhidi ya Ukraine.
Mara nyingi wao hushawishiwa kujiunga na jeshi la Urusi kwa ahadi ya kupewa kazi na ufadhili wa masomo.
Kitengo cha jeshi la Ukraine kinachofahamika kama 57 Motorized Infantry Brigade kilitoa video ya Mkenya aliyejitambulisha kama Evans.
Mkenya huyo alidai kuwa alikuwa mtalii na alihadaiwa kuingia kwenye jeshi la Urusi.
Mwanaume kwenye video hiyo alidai kuwa alikuwa mwanariadha na siku ya mwisho ya ziara yake, maafisa Urusi walimhadaa walikuwa na kazi ya kumpa.
Waliharakisha kumtengenezea stakabadhi hitajika ikiwemo cheti cha kufanyia kazi katika taifa la kigeni. Siku iliyofuata, walimletea karatasi zilizokuwa na maandishi ya Urusi ambazo alizitia saini.
Kisha aliabiri gari lakini maafisa hao wa Urusi hawakumwambia walikokuwa wakimpleka na pia kazi ambayo alikuwa amepata.
Ilibainika stakabadhi alizotia saini zilikuwa za kukubali kujiunga na wanajeshi wa Urusi katika vita dhidi ya Ukraine.
“Walinielekeza mahali pa kutia saini na pa kuandika jina langu kabla ya kuondoka na stakabadhi zenyewe. Wakati huu wote hawakuwa radhi kuniambia aina ya kazi ambayo ningefanya,” akasema akifichua kuwa simu yake na pasipoti yake ya Kenya zilitwaliwa.
“Baadaye nilijipata nje ya kambi ya mafunzo ya kijeshi na wakaniambia nilikuwa nimekubali kuwa mwanajeshi wala singeghairi nia wakati huo. Wakati wa mafunzo hayo, wakuu hao wa kijeshi walikuwa wakizungumza Kirusi na ilikuwa vigumu sana kuwaelewa,” akaongeza.
Evans alifichua kuwa alipewa bastola ili ajiunge na kitengo cha jeshi la Urusi. Alihepa na kuingia kwenye msitu ambako alijisalimisha kwa wanajeshi wa Ukraine eneo la Kharkiv Oblast, karibu na mji wa Vovchansk.
Video hiyo inayothibitisha kuwa Wakenya wanazuiliwa Ukraine inafuata tukio la Agosti 2023 ambapo mwanafunzi raia wa Uganda Habil Bosco Magara aliuawa. Kifo chake kilitokea akiwa vita na wanajeshi wa Urusi dhidi ya Ukraine. Magara alikuwa na ufadhili wa masomo Urusi ambapo alikuwa akisomea Sayansi ya Kompyuta.
Lemekani Nathan Nyirenda, mwanafunzi raia wa Zambia, aliuawa mnamo Septemba 2022 akipigania Urusi.
Mauti yao yamezua maswali iwapo Urusi inatumia ufadhili wa masomo kuwashawishi Waafrika kuungana na jeshi lao katika vita dhidi ya Ukraine.
Taifa Leo imebaini kuwa kuna raia wa Afrika ambao wako kambi ya jeshi Kyiv baada ya kuhadaiwa kuwa wangepewa ufadhili wa masomo. Raia hao wanatoka Togo, Ghana, Somalia, Sierra Leone, Egypt na Tunisia.