Raila ni mzima, hajaenda ng’ambo kusaka matibabu, Afisi Kuu ya ODM yatangaza
SEKRETARIATI ya Raila Odinga Jumapili ilikanusha ripoti kuwa afya ya aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga i taabani ikisema kuwa ni habari zinazosukumwa na kuenezwa kukiwa na ajenda ya kisiasa.
Msemaji wa Raila, Bw Dennis Onyango aliwashutumu aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua, Kinara Wiper Kalonzo Musyoka na Kiongozi wa DAP-K Eugene Wamalwa kwa kuendeleza kampeni na habari za uongo kuhusu afya ya Raila.
Kwa mujibu wa taarifa ya Bw Onyango, habari hizo zimekuwa zikiendelezwa na viongozi hao ambao walikuwa wakipinga azma ya Raila ya uenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC) mapema mwaka huu.
Aidha sekretariati hiyo ilikashifu wanasiasa hao kwa kutumia vyombo vya habari, mabloga na picha zilizoundwa kupitia Akiliunde (AI) kufahamisha umma kuwa Raila anachungulia kaburi.
“Lengo la viongozi hawa ni kumshurutisha Raila ajiunge na mrengo wao katika kuendeleza maasi dhidi ya Rais William Ruto,” akasema Bw Onyango.
Aliongeza kuwa Raila mara si moja amekuwa na uwazi kuhusu afya yake na mara si moja amefahamisha umma kuhusu matibabu yake akiugua.
“Akiwa waziri mkuu mnamo Juni 2010 aliwaambia Wakenya alipokuwa akitibiwa. Vilevile alipokuwa akiugua na akalazwa hospitalini mnamo 2021, aliwafahamisha Wakenya.
“Hadi leo atafanya hivyo, iwapo angekuwa akiugua jinsi ambavyo wapinzani wake wanamtakia,” akasema.
Bw Onyango alifafanua kuwa Raila haugui na aliondoka nchini Ijumaa kwa safari yake Ughaibuni. Alifunguka na kusema kuwa Raila hakusafiri Ulaya jinsi ambavyo baadhi ya mabloga wamekuwa wakieneza.
“Hakuenda Ulaya wala haugui jinsi ambavyo baadhi ya wapinzani ambao wamehangaika wanavyomwombea,” akasema.
Viongozi wa upinzani hawakuwa wamejibu madai ya kudhamini uvumi kuhusu afya ya Raila wakati wa kuchapisha habari hizi.
Kuhusu ushirikiano wake na Rais William Ruto, Bw Odinga hatetereki na ataendelea kuunga Serikali Jumuishi.
“Awe ugenini au nyumbani, Raila bado yuko ndani ya Serikali Jumuishi. Anaamini kuwa umoja na utaifa ni muhimu kuliko maslahi ya kila kiongozi.”

Bw Odinga mnamo Ijumaa kabla ya kusafiri nje ya nchi, alikutana na uongozi wa klabu ya Gor Mahia ambapo alitunuku klabu hiyo Sh10 milioni.
Mapema siku hiyo alikutana na baadhi ya viongozi wa ODM katika hoteli ya Serena ambapo alionekana kuwa mchangamfu mno.