Makala

Kutana na Esther Nyawira, refa mhasibu na mwanamazingira

Na GEOFFREY ANENE October 9th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

CHINI ya jua kali katika makala ya saba ya Raga za Vyuo Vikuu vya Afrika (FASU) yaliyofanyika ugani KCB Ruaraka, Nairobi, refa Esther Nyawira Nyambura,25, anasimama katikati ya uwanja akiwa mtulivu, akitoa amri kwa ujasiri.

“Inahisi vizuri unapokuwa uwanjani ukiwaamrisha wanaume,” anasema kwa tabasamu hapo Oktoba 4, 2025.

Nyambura ni mmoja wa marefa wachache wa kike wa raga nchini Kenya. Kuna marefa wanane pekee wa mchezo huo nchini Kenya. Safari ya Nyambura ilianza katika shule ya Hidden Talent mtaani Dagoretti alipocheza kama nambari tisa (scrum-half), lakini hakuwahi kujitosa katika kucheza raga ya kulipwa.

Baada ya shule, alijaribu ‘baseball’ hadi janga la COVID-19 lilipoibuka, kisha akarudi raga, mchezo alioupenda kwa nidhamu na umoja wake.

Mwaka 2022, Nyambura alianza rasmi kuwa refa, lakini mechi yake ya kwanza ilimvunja moyo. “Wachezaji walitoka nje ya uwanja wakiwa hawajaridhika nami. Nilihisi kuvunjika moyo,” anakumbuka. Hata hivyo, hakukata tamaa. Akiungwa mkono na wakufunzi wa marefa (CMOs) na wenzake, aliendelea kufundishwa na kukua.

Miaka miwili baadaye, Nyambura amechezesha zaidi ya michuano 30, ikiwemo Ligi Kuu ya Wanawake, Ligi ya Daraja la Tatu ya Wanaume, na Raga za Kitaifa za Wachezaji saba kila upande, akisimamia fainali ya kwanza mjini Nakuru wakati wa Prinsloo Sevens na mechi ya medali ya shaba katika Dala Sevens 2025 mjini Kisumu. “Ilikuwa hatua kubwa kwangu,” anasema kwa fahari.

Mwanamazingira Esther Nyambura wakati wa mashindano ya raga ya vyuo vikuu vya Afrika jijini Nairobi. PICHA|GEOFFREY ANENE.

Bidii yake ilimletea tuzo ya Refa Bora Mwanamke anayeinuka 2024–2025. “Sikutarajia kabisa,” akasema. “Lakini nilikuwa nimejituma mazoezini na kupitia video za mechi kila Jumanne, na kuweka malengo na CMO wangu.”

Moja ya kumbukumbu zake bora zaidi ni wakati alipoongoza fainali ya Ligi ya Daraja la Tatu kati ya timu ya NYS na Administration Police, ikiwa ni mechi ya kwanza kabisa nchini Kenya kuchezeshwa na waamuzi wa kike pekee. “Ilikuwa historia. Sikuamini mwanzoni,” akaeleza.

Nje ya uwanja, Nyambura ni mhasibu katika kampuni ya Power Governors Limited inayojihusisha na teknolojia za magari. Ana shahada ya fedha kutoka Chuo Kikuu cha KCA na anapanga kuendelea na masomo ya juu. “Waajiri wangu wananisaidia sana, wananipa nafasi kufanya ninachopenda,” akasema.

Kwa kuwa mechi nyingi hufanyika wikendi, Nyambura anaweza kufanya kazi, kuwa na familia yake, na kufanya uhifadhi wa mazingira. “Ninapenda mazingira, mimea, na kufanya dunia iwe bora,” akasema. Mapenzi haya yalimfanya kuanzisha mradi wa ‘Tries for Trees’, unaounganisha raga na upanzi miti.

“Kila mguso unaofungwa katika mashindano unawakilisha mti mmoja unaopandwa,” anaeleza. Mradi huo umehusisha vyuo, shule na klabu kama Kenyatta University, JKUAT, Zetech, Kabras Sugar RFC na Lenana School, ukiwa na lengo la kupanda miti 50,000 kufikia 2026. “Tunashirikiana na Ngong Forest na Kenya Forest Service ambao hutoa miche,” anasema.

Ndoto yake ni kufika mbali zaidi. “Siku moja nataka kuchezesha mechi nje ya Afrika, na kuona uhusiano kati ya michezo na mazingira ukitambuliwa duniani. Labda tuwe na tuzo kama upanzi wa miti (Sports Trees Award)!” akasema.

Hata hivyo, Nyambura anasema changamoto zipo. “Mchezo wa raga unachukuliwa zaidi kama uwanja wa wanaume, lazima uwe na kiwango sawa cha mazoezi na uthabiti. Watu bado huona ajabu mwanamke akiwa refa, lakini hali inabadilika.”

Kwa Nyambura, kila siku uwanjani ni nafasi ya kuthibitisha kuwa wanawake wanaweza kuongoza mchezo kwa haki, nidhamu, na moyo wa kijani unaopanda miti kama anavyopanda matumaini mapya.