TSC yabatilisha barua ya kuwahamisha walimu waliopandishwa vyeo
TUME ya Kuajiri Walimu (TSC) imebatilisha barua zilizotolewa za kuwahamisha walimu kutoka Nairobi hadi Kitui ikisema ni kinyume na sheria.
Walimu walioathiriwa, ambao walikuwa wamepandishwa vyeo hivi majuzi, walikata rufaa dhidi ya hatua hiyo wakitaja changamoto ikiwa ni pamoja na uzee, matatizo ya kiafya.
Kufuatia rufaa hizo, baadhi ya walimu wamepokea barua za kuthibitisha kwamba upandishaji vyeo unaendelea kuwa halali. Barua hizo pia ziliwahakikishia kuwa wataendelea kuhudumu katika vituo vyao vya sasa hadi nafasi zinazofaa zipatikane ndani ya Nairobi.
‘Tume ilipokea rufaa Septemba 10, 2025, ambapo waathiriwa waliomba kuendelea kuhudumu katika Kaunti ya Nairobi kwa misingi ya matibabu,” mojawapo ya barua inasoma.
Walimu hao ni sehemu ya 23,000 waliopandishwa vyeo na TSC mnamo Mei 2025.
Hata hivyo, wengi walishtuka mnamo Septemba 1 walipopokea barua za kuhamishwa na kutoa idhini watumwe katika kaunti za mbali, miezi michache kabla ya baadhi yao kustaafu.