Habari za Kitaifa

Wimbi la ‘Wantam’ lafika nchini Ushelisheli na kung’oa Rais Ramkalawan

Na MASHIRIKA October 12th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

KIONGOZI wa upinzani, Patrick Herminie, ameshinda kinyang’anyiro cha urais na kumbwaga kiongozi aliye mamlakani, Wavel Ramkalawan katika uchaguzi wa marudio, kulingana na tume ya uchaguzi.

Herminie alijizolea asilimia 52.7 ya kura, huku Ramkalawan akiwahi asilimia 47.3, kwa mujibu wa matokeo rasmi yaliyotangazwa mapema Jumapili.

Katika hotuba yake ya ushindi, Herminie aliahidi kupunguza gharama ya maisha, kufufua huduma za umma na kuunganisha taifa hilo la kisiwani.

“Watu wamezungumza,” alisema Herminie, 62, katika makao makuu ya tume ya uchaguzi.

“Nimesalitika sana kwa imani ambayo watu wameniwekea. Nitakuwa rais wa raia wote wa Ushelisheli, na nitazima migawanyiko kwa kukomesha mapendeleo, na kumpa kila mtu fursa ya kunawiri,” alisema.

Ushindi wa Herminie, aliyewahi kushtakiwa kwa ushirikina mnamo 2023, umekipa chama chake cha United Seychelles udhibiti kikamilifu wa serikali baada ya kunyakua vilevile wabunge wengi bungeni katika awamu ya kwanza ya uchaguzi mkuu mwezi uliopita.

Ushindi huo pia ni mabadiliko makuu kwa Herminie, ambaye 2023 alikamatwa kwa mashtaka ya ushirikina yaliyofutiliwa mbali baadaye. Alihudumu awali kama spika wa bunge la kitaifa kuanzia 2007 – 2016.

Ramkalawan, aliyehudhuria pia hafla ya tume ya uchaguzi kutangaza matokeo, alimpongeza Herminie, ambaye sasa ni rais wa sita wa Ushelisheli.

“Naondoka na rekodi inayowafanya marais wengi waone haya…Natumai Rais Herminie ataendelea kudumisha kiwango sawia,” alisema.

Picha zilizochapishwa na gazeti la Seychelles Nation zilionyesha viongozi hao wawili wakisalimiana baada ya tangazo hilo.

Nje ya makao makuu ya tume, maelfu ya wafuasi wa Herminie walishangilia kwa nderemo na vifijo wakipeperusha bendera ya taifa na mabango ya chama huku wakimsalimia alipotangazwa mshindi, zilionyesha video kwenye mitandao ya kijamii.

Kinyang’anyiro kati ya wagombea wawili wakuu kiliishia marudio baada ya mshindi kukosa kubainika katika uchaguzi wa urais uliofanyika majuma mawili yaliyopita.

Kura ya mapema ilianza Alhamisi, lakini raia wengi nchini walipiga kura Jumamosi.

Herminie na Ramkalawan waliendesha kampeni kali wakijaribu kuangazia masuala nyeti kwa wapigakura, ikiwemo uharibifu wa mazingira na janga la uraibu wa matumizi ya mihadarati katika taifa ambalo kwa miaka mingi limeonekana kuwa kivutio cha watalii.

Ramkalawan alijipigia debe kuchaguliwa kwa hatamu nyingine akiangazia usimamizi wake kwenye ufufuzi wa uchumi kitaifa kutokana na janga la COVID-19 na upanuzi wa mifumo ya kulinda jamii.

Lakini wapigakura walimchagua Herminie, aliyemshutumu Ramkalawan kwa kuruhusu ufisadi, na kuahidi kuvunjilia mbali mkataba wa hoteli ulioruhusiwa na serikali yake ambao watetezi wa mazingira wanasema unahatarisha visiwa vya matumbawe vilivyoorodheshwa na Shirika la Umoja wa Mataifa kuhusu Elimu, Sayansi na Utamaduni, UNESCO.

Herminie vilevile ameahidi kupunguza umri wa kustaafu kutoka miaka 65 hadi 63 na kutekeleza mapendekezo kutoka tume ya ukweli na maridhiano iliyodadisi dhuluma za haki za kibinadamu zinazohusu mapinduzi ya serikali ya 1977 na athari zake.

Akiwa daktari kitaaluma, aliwahi kuongoza asasi ya serikali inayopiga vita mihadarati, na ameahidi kukabiliana na kero sugu la uraibu wa heroni, unaohusishwa kwa sehemu fulani na hali kwamba kisiwa hiki kimekalia mkondo wa kusafirishia mihadarati kati ya Afrika na Bara Asia.

Taasisi ya Kitaifa kuhusu Kuzuia Matumizi ya Mihadarati na Urekebishaji Tabia inasema watu 5,000 – 6,000 hutumia heroini miongoni mwa jumla ya watu 120,000.

Takwimu nyinginezo zinakadiria idadi hiyo kufikia 10,000.

Ushelisheli, taifa linalosheheni visiwa 115, ndiyo nchi tajiri zaidi Afrika.

Inapatikana umbali wa kilomita milioni 1.2 mraba (maili 463,000 mraba) Mashariki mwa Bahari Hindi, ni kivutio kikuu cha watalii pamoja na kituo cha uwekezaji kutoka, na ushirikiano kiusalama na China, mataifa ya ghba na India.