Michezo

Raila Odinga aombolezwa na wanamichezo, alipenda soka sana

Na GEOFFREY ANENE October 15th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

WANAMICHEZO nchini Kenya wanaomboleza kifo cha mmoja wa wafuasi wakubwa wa michezo, Raila Amolo Odinga mnamo Jumatano, Oktoba 15, 2025.

Kiongozi huyo mashuhuri anayejulikana kwa majina kama Tinga, Baba, RAO, na Agwambo, alikuwa shabiki mkubwa wa Gor Mahia, Arsenal inayoshiriki Ligi Kuu ya Uingereza na pia timu ya taifa ya Kenya, Harambee Stars.

Odinga aliaga dunia nchini India alipokuwa akipokea matibabu. Ripoti kutoka India zinasema alizimia wakati wa matembezi ya asubuhi na kufariki.

Shirikisho la Soka Kenya (FKF) limesema linaungana na taifa kuomboleza kifo cha Mheshimiwa Odinga.

“Alikuwa kiongozi mwenye maono na shabiki wa kweli wa kandanda ya humu nchini. Urithi wake utaendelea kuhamasisha vizazi vijavyo. Tunatuma rambirambi zetu kwa familia yake, marafiki, na Wakenya wote katika wakati huu mgumu,” FKF inayoongozwa na Hussein Mohammed, ilisema.

Shirikisho la Raga la Kenya (KRU) pia limesema: “Jumuiya ya raga inaungana na taifa kuomboleza kifo cha Waziri Mkuu wa zamani Raila Odinga. Tunatuma salamu za pole kwa familia yake na Wakenya wote. Mchango wake katika kuijenga Kenya yenye umoja na maendeleo unabaki kuwa mwanga kwetu sote. Kama jamii ya raga, tunaheshimu urithi wake wa uongozi na uzalendo.”

Klabu ya Gor Mahia, ambayo Odinga alikuwa mlezi wake kwa miaka 20, imemuomboleza ikisema: “Mioyo yetu imejaa huzuni kufuatia kifo cha mlezi wetu mpendwa, Mheshimiwa Raila Odinga. Alikuwa nguzo na mwanga kwa klabu yetu. Tunatuma rambirambi kwa familia yake. Pumzika kwa amani Baba.”

Mahasimu wa tangu jadi wa Gor, AFC Leopards nao wamehuzika na kifo cha kiongozi huyo aliyesaidia klabu hizo mara kadhaa kifedha.

“Kiongozi shupavu na shabiki mkubwa wa kandanda. Pumzika kwa amani Mheshimiwa Raila Odinga,” Leopards ikasema.

Waziri wa Michezo, Salim Mvurya, amesema taifa limepoteza nguzo kubwa ya uongozi.

“Raila alikuwa mtu mwenye ujasiri, maono, na imani isiyotetereka katika demokrasia ya Kenya. Natoa rambirambi zangu kwa Mama Ida Odinga, familia ya Odinga, marafiki, na Wakenya wote. Raila alikuwa mwalimu kwa wengi, akiwemo mimi, na alijitolea kupigania ugatuzi, usawa, na taifa lenye umoja. Urithi wake wa uvumilivu, kujitolea na uzalendo utaendelea kuongoza safari ya kidemokrasia ya Kenya.”

“Inna lillahi wa inna ilayhi raji’un.”