Walanguzi watumia matineja kusafirisha dawa za kulevya
MAAFISA wa upelelezi wa Jinai (DCI) Kaunti ya Meru, wanachunguza kisa ambapo walanguzi wa bangi wanawatumia wavulana matineja kusafirisha dawa za kulevya.
Hii ni baada ya maafisa hao kuwanasa vijana wawili walioabiri matatu katika kituo cha Tea Room Nairobi wakielekea Maua, Kaunti ya Meru. Wawili hao walifika katika kituo hicho wakiwa na mikoba kama wanafunzi.
Gari hilo lilipofika katika Ofisi ya Upelelezi wa Jinai Kaunti ya Meru, maafisa wa polisi walipata misokoto 25 ya bangi yote ikiwa na uzito wa kilo 75.
Kulingana na polisi bangi hiyo ina thamani ya Sh750,000.
Mkurugenzi wa Kampuni ya Maua Shark Express Moses Kinyua alisema abiria hao wawili walifika kwenye kituo cha Tea Room kwa pikipiki na kupanda matatu.
“Wafanyikazi wetu hawakujua ni nini kilikuwa kwenye mizigo hadi gari hilo lilipozuiliwa na polisi Meru. Inaonekana walanguzi hao wamekuwa wakitumia njia hizi kusafirisha dawa zao,” Bw Kinyua alisema.
Kamanda wa Kaunti ya Meru Patrick Labolia alisema wamepokea taarifa za kijasusi kutoka kwa umma kwamba matatu kadhaa zinazoelekea Meru zilikuwa zikitumika kusafirisha bangi.
“Tunafurahia uhusiano wetu mzuri na ushirikiano wetu na umma, maafisa wetu walipata habari abiria walipopanda matatu. Duru zetu zilidokeza kuwa wafanyabiashara wa dawa za kulevya walikuwa wakitumia njia hiyo kusafirisha bidhaa yao. Hata hivyo, tulifaulu kunasa shehena moja,” Bw Labolia alisema.
Alisema wahusika hao wenye umri wa miaka 15 na 17 walikuwa wamebeba vifurushi hivyo kwenye mikoba ya shule kama njia ya kuficha.
Bw Labolia alisema maafisa wa upelelezi sasa wanamsaka mwenye bidhaa hizo baada ya kukusanya taarifa za kijasusi kutoka kwa washukiwa hao wawili ambao sasa wako kizuizini.
Kamishna wa Kaunti ya Meru Jacob Ouma alisema visa hivyo vimeenea katika eneo hilo. Bw Ouma alisema bangi na ethanol ndizo zinazouzwa zaidi ndani na nje ya kaunti.
“Inasikitisha kwamba walanguzi wa dawa za kulevya wanatumia watoto wadogo katika biashara yao chafu. Tumetoa onyo kali kwa maafisa wa usalama dhidi ya kula nja au kuendeleza biashara hii haramu katika kaunti,” Bw Ouma alisema. Aliongeza, “Utumiaji wa dawa hizo huchochea mimba za mapema, ukatili wa kijinsia, unajisi na vurugu katika familia.”