Habari za Kitaifa

Mwili wa Raila watua uwanja wa Mambo Leo, Kisumu

Na BENSON MATHEKA October 18th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

Mwili wa aliyekuwa Waziri Mkuu wa zamani, Raila Odinga, umefika katika Uwanja wa Mamboleo, Kisumu, ambako maelfu ya watu wamekusanyika kutoa heshima zao za mwisho kwa kiongozi huyo mashuhuri.

Shughuli hii ilianza asubuhi ya Jumamosi, Oktoba 18, 2025, mara tu baada ya ndege ya kijeshi iliyobeba mwili wake kutua katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kisumu. Kutoka hapo, mwili wake ulisafirishwa kwa helikopta hadi Mamboleo kutazamwa na umma.

Maelfu ya waombolezaji kutoka eneo la Nyanza walijitokeza mapema wakiwa wamevalia mavazi ya huzuni, kuonyesha upendo wao kwa Raila Odinga. Uwanja huo umejaa hisia nzito huku watu wakiimba nyimbo za maombolezo na kumbukumbu.

Baada ya shughuli ya leo kumalizika, mwili wa Raila utasafirishwa kwa barabara hadi kwao Bondo, Kaunti ya Siaya, kwa mazishi yatakayofanyika Jumapili, Oktoba 19, 2025.

Maandalizi ya mapokezi ya mwili huo yalifanywa Ijumaa, kwa ushirikiano kati ya Jeshi la Ulinzi la Kenya (KDF), maafisa wa serikali, viongozi wa eneo hilo na wananchi. Naibu Rais Kithure Kindiki, ambaye ni mwenyekiti wa kamati ya maandalizi ya mazishi, aliwahimiza wananchi kuwa wameketi kufikia saa moja asubuhi ili kuhakikisha shughuli zinaendelea kwa heshima na utulivu.