Habari Mseto

Vitisho vya magaidi kuvamia Kiganjo, Nyeri na Nanyuki vyachunguzwa

February 19th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na NICHOLAS KOMU

USALAMA umeimarishwa eneo la Mlima Kenya kufuatia ripoti kwamba magaidi wanapanga kushambulia Chuo cha Mafunzo ya Polisi kilichoko Kiganjo na makanisa kadhaa katika Kaunti ya Nyeri.

Maafisa wa usalama walitoa tahadhari ya shambulizi la kigaidi huku uchunguzi ukiendelea kufuatia habari hizo.

Kamishna wa Kaunti ya Nyeri, Fredrick Shisia, Jumanne aliambia Taifa Leo kwamba mashirika kadhaa ya usalama yanaendelea kuchunguza vitisho hivyo.

“Kumekuwa na vitendo vya kigaidi ambavyo vimekabiliwa kufikia sasa. Mashirika husika yanaendelea kuchunguza vitendo hivyo na vilipoanzia,” alisema Bw Shisia.

Kulingana na duru za polisi, vitisho vya kwanza vilipokelewa Jumamosi vikidai kwamba kungekuwa na mashambulizi katika makanisa kadhaa ambayo hayakutajwa katika Kaunti ya Nyeri.

Kufuatia habari hizo, usalama uliimarishwa katika maeneo ya kuabudu katika kaunti hiyo.

Jumatatu usiku, polisi waliongeza doria mjini Nyeri baada ya wapelelezi kupata habari kwamba Chuo cha Kitaifa cha Mafunzo ya Polisi kilichoko Kiganjo kingeshambuliwa.

Maafisa wa polisi walitumwa kwa wingi kupiga doria karibu na chuo hicho katika juhudi za kuzuia shambulio hilo. Polisi walisema walikuwa wakichunguza chanzo cha habari hizo.

Hakuna aliyekamatwa kuhusiana na vitisho hivyo lakini Bw Shisia alisema wanafuatilia habari muhimu.

“Hili ni suala tunaloendelea kuchunguza tunapoimarisha usalama. Baadhi ya vitisho hivi vinalenga asasi muhimu kama taasisi za masomo na makanisa na maafisa wetu wanafanya kila wawezalo kuzuia shambulio la aina yoyote,” alisema Bw Shisia.

Ripoti za tisho hilo zilijiri siku chache baada ya mwanafunzi kukamatwa akiwa na vifaa vilichoshukiwa kuwa vilipuzi karibu na Chuo Kikuu cha Teknolojia cha Dedan Kimathi.

Bruce Ndegwa, ambaye anazuiliwa na polisi kwa siku saba kufuatia agizo la mahakama, alikuwa amejifunga vifaa hivyo mwilini, kiunoni na kifuani.

Usalama pia umeimarishwa mjini Nanyuki katika Kaunti ya Laikipia baada ya tisho la kigaidi kuripotiwa katika eneo ambalo halikutajwa.

Kamishna wa Kaunti hiyo Onesmus Musyoki alithibitisha kuwa polisi wanachunguza vitisho hivyo lakini hakufichua zaidi.

“Kumekuwa na vitisho, baadhi ni uvumi lakini tunazichukulia kwa uzito sana. Uchunguzi unaendelea kuhusu habari tulizopokea,” alisema Bw Musyoki.