Jamvi La Siasa

Haiyaa, kitendawili hadi tibim, Raila azikwa na ucheshi wake

Na BENSON MATHEKA October 19th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

KAMPENI za kisiasa za Raila Odinga zilipambwa kwa ucheshi, nyimbo, vitendawili na semi zilizochangamsha.

Kuanzia kwa vitendawili maarufu hadi kwa kubuni matangazo akifananisha uchaguzi na mechi ya soka kati ya mrengo wake na washindani, Raila alibadilisha mikutano ya kisiasa kuwa ya kusisimua.

Katika kila mkutano mkubwa, umati ulisubiri atoe “Kitendawili!” Nao ulijibu, “Tega!” Kisha kitendawili kilifuata, mara nyingi kikiwa na maana ya kisiasa.

Mwaka wa 2017, katika mojawapo ya matamshi yake ya kukumbukwa, atumia methali, “Kelele za chura haziwezi kuzuia ng’ombe kunywa maji.”

Mnamo Juni 25, 2017 akiwa Busia, alitumbuiza umati kwa kitendawili kilichobeba kejeli kali ya kisiasa:

“Kitendawili… Tega! Alikimbia usiku uchi akachoka akalala fo fo fo. Alipoamka asubuhi alipata aibu kubwa. Yeye ni nani? Mmeshindwa. Mnipatie mji, eti Busia?Huyo ni mchawi, huyo ni Jubilee. Miaka nne wamelala fofofo.”

Mbali na kuchekesha, vitendawili vyake vilijaa ujumbe kuhusu siasa, uvumilivu na matumaini.

Raila alielewa jinsi mpira wa miguu ulivyo na mvuto kwa Wakenya. Mwaka wa 2017, aligeuza hotuba zake za kisiasa kuwa maelezo ya mechi. Umati ulifurahia aliposema:

“Pande ile Uhuru ameanza, amepatia Ruto, Ruto anampatia Duale… Kindiki amepiga shuti, mpira i(u)meenda nje!”

“Mpira unarudi kwa Weta, anampa Isaac Rutto, amechenga William Ruto hadi ameanguka. Mpira bado unaenda mbele…”

“Musalia Mudavadi anapewa, anachenga Duale, anampatia Kalonzo, Kalonzo anampa Raila… GOOOAAAL!”

Kauli mbiu ya Raila ya mwaka wa 2022, “Inawezekana,” iliibua matumaini. Ilionekana kwenye mabango, fulana na nyimbo. Alipoitumia pamoja na “Leo ni Leo,” alizidisha ari miongoni mwa wafuasi wake kwamba ushindi ulikuwa karibu.

Mwaka wa 2013, Raila alitumia kauli “Punda Amechoka” kuonyesha kuchoshwa kwa wananchi na ufisadi na uongozi mbaya.

Mwaka 2017 alikumbatia maneno Tibim na Tialala yaliyozinduliwa na viongozi vijana kama Babu Owino na kuingia rasmi kwenye kampeni za Raila..

Hayaaa! Kabla ya kuanza kampeni zake, Raila alianza kwa tamko maarufu “Hayaaa!”. Alipotamka neno hili, umati ulitulia mara moja, ukisubiri kauli muhimu. Kwa wafuasi wake, lilikuwa ishara kwamba jambo la maana linafuata.

Kwa Raila, siasa hazikuwa tu kuhusu kura, bali kuhusu kuwasiliana. Maneno yake yaliwafikia watu wa kawaida. Alizungumza lugha yao, alicheza nyimbo zao, na alielewa matumaini yao. Alitoa siasa kwa viongozi na kuirudisha kwa wananchi.

Anapozikwa leo, ucheshi, busara na kauli zake zitabaki kuwa sehemu ya historia ya siasa za Kenya.