Jamvi La Siasa

Siasa za ubabe ODM

Na CHARLES WASONGA October 19th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

NUSRA Mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino abubujikwe na machozi katika mkutano maalum wa Baraza Kuu la Kitaifa (NEC) la ODM Alhamisi aliposhambuliwa kwa kutumia kifo cha Raila Odinga kudhihirisha ubabe wake kisiasa.

Kisa na maana ni kwamba mnamo Jumatano, alidaiwa kuchochea kundi la vijana kutoa kauli za kumsifia nje ya lango la makazi ya Hayati Odinga, mtaani Karen, Nairobi.

Kundi hilo la wafuasi wa ODM walifurika hapo baada ya kutolewa kwa habari kuhusu kifo cha waziri huyo wa zamani na Rais William Ruto na viongozi wengine wapolifika nyumbani kwa mwendazake kumpa pole mjane Ida Odinga.

Lakini Babu, mbunge machachari, aliyeongea kwa huzuni kuu, alijiondolea lawama akitaja madai hayo kama “yasiyo na msingi na yenye kunikosea heshima.”

“Mbele ya Mungu, nitakuwa mtu wa mwisho kuboronga heshima ya Baba. Raila ni mlezi wangu kisiasa na siwezi kufanya kitu kama hicho baada ya kifo chake na anapoombolezwa nchini na kimataifa,” akasema.

Kulingana na Babu, alipoondoka nyumbani kwa Raila, baada ya viongozi wengine wakuu kuondoka, wafuasi waliokuwa wamepiga kambi hapo walianza kupiga kilele wakimsifia.

Hii, alieleza, ilifasiriwa visivyo na baadhi ya viongozi kwamba ni yeye alipanga kuvuna kisiasa kutokana msiba huo mkubwa.

Babu Owino anayehudumu kwa muhula wa pili kama Mbunge, ametangaza azma ya kuwania ugavana wa Nairobi katika uchaguzi mkuu wa 2027. Hii ni kinyume cha matamanio ya Hayati Odinga ambaye, wakati wa uhai wake, alitangaza kuwa chama cha ODM kitamuunga mkono Gavana wa sasa Johnson Sakaja katika kinyang’anyiro hicho.

Lakini mwanasiasa huyo, anayepinga serikali jumuishi inayoshirikisha chama chake cha ODM, aliazimia kuwania wadhifa huo hata bila uungwaji mkono wa uongozi wa chama cha chungwa.