Mashujaa Day 2025: Rais Ruto amtambua Raila kama Shujaa
SIKU moja baada ya taifa kumuaga aliyekuwa Waziri Mkuu, Raila Odinga, Rais William Ruto ameongoza taifa kumtambua mwanasiasa huyo kama Shujaa wa Kenya.
Akihutubu katika maadhimisho ya Mashujaa Dei mwaka huu, 2025, yaliyofanyika Kaunti ya Kitui, Jumatatu, Oktoba 20, Rais Ruto alitenga sekunde kadhaa za kimya – kama njia mojawapo kutambua Bw Odinga.
Waziri Mkuu huyo wa zamani, alifariki juma lililopita, Oktoba 15 akiwa na umri wa miaka 80, katika Hospitali ya Devamatha, Koothattukulam, nchini India ambako alikuwa akipokea matibabu.
Rais Ruto akihutubia taifa kuadhimisha Makala ya 15 ya Mashujaa (Chini ya Katiba ya 2010), alimmiminia sifa Raila Odinga akisema amepigania kwa muda mrefu maslahi ya Wakenya.
“Alipigania na kutetea Kenya – kuhakikisha kwamba kila mwananchi analindwa,” Dkt Ruto alisema.
Mashujaa Dei, siku ambayo hapo awali ilijulikana kama Siku ya Kenyatta, huadhimishwa kila mwaka kutambua Wakenya wenye michango tofauti kwa taifa – kulikuza, boresha na hata waliopigania uhuru wa Kenya.
Kwenye hotuba ndefu iliyotambua Bw Odinga, Rais alisema Waziri Mkuu huyo wa zamani aliweka mbele maslahi ya Kenya licha ya kuwa alipitishwa mengi na dhuluma.
Alitumia mfano wa chaguzi kuu za awali, ambapo Raila Odinga amewania urais mara tano bila kufanikiwa, akisema kiongozi huyo wa ODM aliweka kando tofauti za kisiasa licha ya kuwa baadhi ya chaguzi alikuwa akidai kusheheni wizi wa kura na udanganyifu, na kuamua kukubali matokeo.
“Mwaka uliopita, joto la kisiasa lilipokuwa limepanda na maandamano kutishia Kenya, niliwasiliana na viongozi kadha wa kisiasa na Raila Odinga aliitikia ombi langu. Alinisaidia kuokoa nchi dhidi ya machafuko,” alisema Ruto.
Rais alikuwa akirejelea maandamano ya vijana wa Gen Z ambao 2024 walifanya maandamano ya kifaifa kupinga kupitishwa kwa Mswada wa Fedha 2024 – Sheria ambayo Ruto alilazimika kuitupilia mbali.
Vilevile, kizazi cha Gen Z kilikuwa kikikosoa pakubwa utawala wa serikali ya Kenya Kwanza inayoongozwa na Dkt Ruto. Maandamano hayo, pamoja na ya mwaka huu, 2025, yalisababisha maafa ya mamia ya vijana idara ya polisi ikilaumiwa kwa kuwateka nyara.
Rais Ruto alisema ni kupitia mapenzi ya Bw Odinga kwa taifa, nchi ilitulizwa. Raila Odinga alizikwa mnamo Jumapili, Oktoba 19 nyumbani kwake Kaunti ya Siaya katika hafla iliyoongozwa na Rais Ruto.
Aidha, alipewa mazishi ya kitaifa na mizinga 17 ya kijeshi kufyatuliwa kama dhima kwa kiongozi ambaye amewahi kuhudumu kama Waziri Mkuu. Bw Odinga, ataendelea kuombolezwa kwa muda wa siku saba – tangu alipofariki.