Habari

Babake Njagi alilia Uganda iachilie mwanawe

Na Steve Otieno October 24th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

BABAKE mwanaharakati Bob Njagi, amelilia serikali ihakikishe kuwa mwanawe anarejea Kenya salama akisema tangu atekwe nyara nchini Uganda hajapata amani wala lepe la usingizi.

Bob na Mwanaharakati mwenzake Nicholas Oyoo walitekwa nyara nchini Uganda mnamo Oktoba 1.

Ni muda wa wiki tatu tangu wawili hao watekwe nyara na juhudi za kuhakikisha kuwa wanapatikana na kurejeshwa Kenya zimeambulia patupu.

Mzee Frank, 84 akionekana kuwa na macho mekendu kutokana na kukosa usingizi, asema kuwa kila siku ombi lake ni kwamba amwone mwanawe tena lakini siku zinavyosonga ombi hilo bado halijatimia.

Japo nafsi yake inamwambia kuwa mwanawe bado yupo salama, kinachomsikitisha zaidi ni kuwa hadi sasa serikali za Uganda na Kenya bado hazijazungumzia kutekwa kwa Mabw Njagi na Oyoo.

Rekodi za mahakama zinaonyesha kuwa Mabw Njagi na Oyoo walistahili kufikishwa katika Mahakama Kuu ya Uganda mnamo Oktoba 21 kwenye kesi ambayo iliwasilishwa kortini ili kushurutisha serikali ya Uganda iwaachilie.

Lakini siku hiyo ilipofika, wawili hao hawakufika kortini.

Badala yake jibu liliwasilishwa na Kamanda wa Jeshi la Uganda Silas Kamanda likisema kuwa hawakuwa wakizuiliwa na wanajeshi.

“Tunathibitisha kuwa Nicholas Oyoo na Bob Njagi hawako mikononi mwa jeshi la Uganda na hatujui mahali waliko,” akasema.

Aliongeza kuwa UPF iliangalia rekodi zake na za seli za kuwazuilia wahalifu na wawili hao hawakupatikana.

Ufichuzi huu mahakamani ulidhoofisha zaidiu matumaini ya babake Njagi na wanafamilia wengine kwa sababu waliofikiri walikuwa wakiwazuilia mwanao walikanusha kufahamu waliko.

“Sidhani kuwa Njagi na Oyoo wamefariki. Nafsi yangu imenishawishi kuwa wapo hai, wanazuiliwa mahali na watarejea nyumbani,” akasema Mzee Frank nyumbani kwake Kitengela, Kaunti ya Kajiado.

Mzazi huyo licha ya ukongwe wake na msongo wa mawazo anaoupitia, ameshikilia kuwa ana wingu la matumaini la kumwona mwanawe akiwa hai.

Mashirika ya Kijamii nayo yamekuwa yakipambana ili kuhakikisha wawili hao wanawaachiliwa.

Siku ambayo wawili hao hawakufikisha mahakama ya Uganda, Shirika la Kimataifa la Amnesty lilijiunga na Chama cha Mawakili Nchini (LSK) pamoja na Shirika la Vocal Afrika kushurutisha serikali ya Uganda iwaachilie huru wawili hao.

“Shirika la Amnesty, LSK na Vocal Africa pamoja na mashirika mengine yanatoa wito kwa raia ulimwenguni watie saini barua iliyoandikwa kwa Rais Yoweri Museveni ili Njagi na Oyoo wawaachiliwe.”

Tukio la wawili hao kutekwa nyara Uganda linakuja baada ya serikali ya Kenya kukashifiwa kwa kumnyaka Kizza Besigye akiwa nchini mwaka jana kisha kumkabidhi kwa serikali ya Uganda.