Utafiti: Mbegu za wanaume huanza kudorora kuanzia miaka 30
WANASAYANSI wamebaini umri halisi ambao ubora wa mbegu za kiume huanza kudorora, hali inayoongeza uwezekano wa wanaume kuwarithisha watoto wao mabadiliko ya kijeni yanayosababisha magonjwa mbalimbali.
Utafiti mpya uliochapishwa mwezi huu katika jarida la Nature unaonyesha kuwa wanaume wanaochelewesha kupata watoto hadi wanapofikisha miaka ya mapema ya 30 wana uwezekano mkubwa zaidi wa kupitisha mabadiliko hatari ya kijeni kwa watoto wao.
Kikosi cha watafiti kutoka Uingereza kilitumia teknolojia ya hali ya juu kuchanganua Msimbo-jeni (DNA) kuchunguza zaidi ya sampuli 1,000 za mbegu kutoka kwa wanaume 81 wenye umri wa kati ya miaka 24 na 75.
Utafiti huo uliopewa jina “Sperm sequencing” unafafanua kwamba mabadiliko ya vinasaba katika chembechembe za uzazi yanaweza kurithishwa kwa watoto.
“Kwa binadamu, uteuzi chanya wa mabadiliko katika kipindi cha uzalishaji wa mbegu unaweza kuongeza idadi ya watoto wanaozaliwa na magonjwa fulani ya ukuaji,” inasema ripoti hiyo.Uchambuzi wa DNA ulionyesha kuwa asilimia 2 ya mbegu kutoka kwa wanaume wenye umri wa miaka 30 tayari zilikuwa na mabadiliko hatari yanayohusishwa na magonjwa ya watoto.
Kiwango hiki kiliongezeka sana kadri ya umri, kikipanda hadi kati ya asilimia 3 na 5 kwa wanaume wenye umri wa miaka 43 hadi 74, huku wale wa miaka 70 wakiandikisha asilimia 4.5 ya mabadiliko hatari kwenye mbegu zao.
Watafiti walisisitiza uhusiano wa moja kwa moja kati ya umri wa baba na hatari ya jeni kwa watoto wake, wakihimiza wanaume wanaopanga kupata watoto kutathmini matokeo haya.
“Tumeonyesha kuwa mchakato wa uzalishaji wa mbegu huongeza mara mbili au tatu uwezekano wa mabadiliko ya vinasaba vinavyosababisha magonjwa na kusababisha hadi asilimia 5 ya mbegu za wanaume wa umri wa kati hadi wazee kubeba mabadiliko hatari,” waliandika wanasayansi.
Watafiti walieleza kuwa ongezeko la mabadiliko haya hatari halisababishwi tu na makosa ya DNA yanayojitokeza kwa muda, bali pia na mchakato wa kiasili wa ndani ya korodani unaotoa nafasi ya kuendelea kwa baadhi ya mabadiliko fulani ya vinasaba.
Wataalamu wanataka utafiti wa kina zaidi ufanywe kubaini jinsi afya ya watoto inavyoathiriwa na ongezeko la mabadiliko ya vinasaba katika mbegu za wanaume.