Makala

Hayati Raila asilaumiwe kufanya handisheki na Ruto

Na WINNIE ONYANDO October 24th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

MWENYEKITI wa kamati ya uchaguzi wa vuguvugu la Bunge la Mwananchi, Robert Kiberenge amesema Wakenya hawafai kumlaumu aliyekuwa Waziri Mkuu wa zamani, hayati Raila Odinga, kwa kufanya handisheki na Rais William Ruto, akisema hatua hiyo ilikuwa ya kimkakati kama ilivyokuwa mwaka 2000.

Akizungumza na Taifa Dijitali, Bw Kiberenge alisema wengi wanakosea kwa kumhukumu Raila hasa walipoona akilegeza msimamo wake dhidi ya serikali ya Kenya Kwanza.

“Kama taifa, tuliharakisha kumhukumu Raila kwa usaliti. Wengi walidhani amepoteza mwelekeo kisiasa, lakini mimi niliona mbinu ya muda mrefu, kama ile aliyotumia mwaka 2000 alipoingia katika ushirikiano na Hayati Rais Daniel arap Moi kupitia KANU,” alisema.

Alisema hatua hiyo ya Raila miaka 23 iliyopita ilionekana kama usaliti, lakini baadaye iligeuka kuwa silaha ya kisiasa iliyobadili historia ya Kenya.

“Wakati huo, Raila alitumia ushirikiano huo kuvuruga KANU kutoka ndani, jambo lililosababisha kuundwa kwa muungano wa NARC uliomaliza utawala wa KANU wa miaka 39,” akasema.

Kwa mujibu wa Bw Kiberenge, Raila hakuwahi kufanya siasa za kawaida. “Kila hatua yake ilikuwa na maana fiche. Watu walimwona kama amenyamaza au amechoka kisiasa, lakini mimi nilijua alikuwa akicheza mchezo wa kimkakati,” aliongeza.

Alisema hata baada ya maridhiano ya mwaka 2023 na Rais Ruto, hakuwahi kumkosoa Raila hadharani.

“Nilikemea serikali ya Kenya Kwanza, nilizungumzia hali jinsi gaharama ya maisha ilivyopanda na kukosa kutekeleza ahadi, lakini sikuwahi kumtaja Raila. Sio kwa uoga, bali kwa imani kwamba alikuwa na mpango,” alisema.

Bw Kiberenge alisema kifo cha Raila kimeacha pengo kubwa kisiasa na kihisia.

“Tumempoteza mtu ambaye hakuwahi kuishi maisha ya kawaida ya mwanasiasa. Alikuwa taasisi, historia na ndoto ya kizazi kizima cha Wakenya waliotamani haki na usawa,” alisema kwa huzuni.

Aliongeza kuwa taifa halitawahi kujua kile ambacho Raila alikuwa amepanga.

“Pengine alikuwa na mpango maalum kuelekea uchaguzi wa 2027. Baba ameenda, lakini wazo lake la Kenya yenye usawa na haki halijazikwa,” akasema.

Raila, ambaye alikuwa kiongozi wa muda mrefu wa upinzani na mmoja wa wanasiasa wenye ushawishi mkubwa Afrika, alifariki Oktoba 15, 2025 India.

Mazishi yake yalihudhuriwa na viongozi wa kitaifa, wa kimataifa na maelfu ya wananchi waliomfahamu kama “Baba wa Demokrasia.”