Michezo

Sina shaka Salah atapata makali yake tena, asema Slot kuelekea mechi ya Brentford

Na GEOFFREY ANENE October 24th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

KOCHA wa Liverpool, Arne Slot, amesema Ijumaa, Oktoba 24, 2025, kuwa hana wasiwasi kuhusu uwezo wa mshambulizi matata Mohamed Salah kupata makali yake tena ya kufunga mabao, akiamini changamoto zake za sasa zinaweza kutokana na Trent Alexander-Arnold kujiunga na Real Madrid.

Salah na Trent walishirikiana vizuri sana pembeni kulia mwa Liverpool kwa miaka mingi kabla ya Trent kununuliwa na Madrid mwishoni mwa msimu uliopita.

Tangu wakati huo, Salah amefunga mabao mawili tu katika mechi nane za Ligi Kuu msimu huu na ameonekana kupoteza mwelekeo. Alianzishwa kwenye benchi dhidi ya Eintracht Frankfurt katika Klabu Bingwa Ulaya hapo Oktoba 22 wakati kikosi kilichobadilishwa sana cha Reds kilishinda 5-1.

Liverpool watacheza na Brentford ligini hapo Oktoba 24, na uchaguzi wa kikosi cha Slot unatarajiwa kuzua mjadala.

Akizungumzia sababu za Salah kupungukiwa na mabao, Slot amesema wachezaji hukosa nafasi na ni jambo la kawaida, lakini hana shaka Salah ataanza kufunga tena kwa sababu amekuwa mfungaji bora maisha yake yote.

Kocha huyo Mholanzi ameongeza kuwa labda kutocheza tena na Trent, ambaye alikuwa naye kwa muda mwingi Liverpool, kuna athari, na sasa wanatafuta uhusiano mpya ndani ya timu.

Nafasi ya Salah kucheza dhidi ya Brentford imeongezeka kwani mvamizi matata wa Uswidi, Alexander Isak huenda akaukosa mchezo kutokana na jeraha la paja, huku Alisson Becker na Ryan Gravenberch pia wakiwa mashakani. Jeremie Frimpong hatacheza wiki hii wala ijayo kwa sababu ya jeraha la misuli.

Ushindi dhidi ya Frankfurt nchini Ujerumani ulihitimisha kipigo cha mechi nne mfululizo kwa Liverpool. Slot amesema timu yake imekuwa ikiadhibiwa kwa kila kosa dogo, na sasa wanahitaji kucheza kwa ukamilifu kila mara ili kuepuka kuadhibiwa tena.

Imetafsiriwa na Geoffrey Anene