Pambo

Kuomba msamaha katika ndoa si udhaifu

Na WINNIE ONYANDO October 27th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

KAMA vile tunavyoelezwa katika kitabu cha Mhubiri 3:1-8: Kila kitu kina majira yake, hivyo basi kuna wakati wa raha na wa kulia katika ndoa.

Kuna wakati ambapo wanandoa watakosana na kumlazimisha mmoja kusema maneno ya kuumiza mwenzake moyo.

Kuna wengine wanaposhikwa na hasira, basi hata hawana muda wa kuchuja maneno yao.

Maneno yasipochujwa, huleta mgogoro katika ndoa.

Hapo ndipo utakapomsikia mwanamke akimkumbusha mume wake maneno aliyoyasema miaka 10 iliyopita.

James Oringa, mshauri wa masuala ya ndoa anasema uwezo wa kuomba msamaha ni nguzo muhimu katika kudumisha amani na mapenzi.

Kutoomba msamaha, au kujifanya wewe ndiye wa kusema kila wakati, ni sumu inayoweza kuua ndoa taratibu bila hata wanandoa kutambua.

Bw Oringa anasema msamaha ni kama dawa inayotibu magonjwa mengi katika ndoa.

“Kila mtu hukosea. Lakini uwezo wa kukiri kosa na kuomba msamaha kwa unyenyekevu huonyesha ukomavu wa kihisia. Wapenzi wanaojua kuomba na kusamehe hujenga uaminifu na kuimarisha uhusiano wao,” anasema Bw Oringa.

Kwa upande mwingine, baadhi ya wanandoa kuchukulia suala la kuomba msamaha kama ishara ya udhaifu.

“Mume au mke akiomba msamaha atahisi kuwa anashusha hadhi yake. Hata hivyo, kuomba msamaha ni kitendo cha ujasiri, si udhaifu. Ni ishara kwamba unathamini amani kuliko vurugu.”

Mshauri huyo pia anasema kuwa msamaha huzuia mambo madogo kugeuka milima mikubwa katika ndoa.

“Kwa mfano, mume akichelewa kurudi nyumbani bila kumjulisha mke wake, anaweza kuomba msamaha na kueleza sababu. Badala ya mke kuhisi kudharauliwa, atahisi kuthaminiwa. Vivyo hivyo, mke anapokosea, labda kwa maneno ya kukera au uamuzi bila ushauri basi akiomba msamaha uhusiano wao utaimarika.”

Naye mwanasaikolojia Caxton Ouma, anasisitiza kuwa kuomba msamaha hakutoshi tu — bali lazima kuwe na mabadiliko ya tabia na mienendo.

“Kama unaomba msamaha lakini unarudia kosa lile lile, basi maneno yako hayana maana. Msamaha wa kweli huambatana na kujitahidi kubadilisha mienendo,” anaeleza.

Zaidi ya hayo, wanandoa wanapaswa kujifunza pia kusamehe.

Baadhi ya watu hukubali kwa maneno lakini moyoni, wanabaki na kinyongo.

Hali hii hujenga ukuta wa kimya unaovuruga mawasiliano.

Kwa ujumla, kuomba msamaha kunapunguza migogoro, kunaleta utulivu, na huimarisha heshima kati ya wanandoa.

Ndoa si uwanja wa kushindana, bali ni safari ya kujenga umoja na amani.

Kwa hivyo, unapokosea, usione haya kusema pole. Neno hilo dogo linaweza kuokoa ndoa yako, kurudisha tabasamu na kudumisha mapenzi.