Polisi sasa mbioni kusaka wamiliki wa mihadarati iliyonaswa
KIKOSI cha Polisi wa Kupambana na Mihadarati kinachunguza simu saba za mkononi zilizopatikana kutoka kwa raia sita wa Iran waliokamatwa katika Bahari Hindi wakiwa na dawa za kulevya aina ya Methamphetamine zenye thamani ya Sh8.2 bilioni.
Hati zilizowasilishwa katika Mahakama ya Shanzu zinaonyesha kuwa, serikali inapanga kufanya uchunguzi wa kimaabara wa simu na kifaa cha GPS zilizopatikana kutoka kwa Jasem Darzaen Nia, Nadeem Jadgai, Imran Baloch, Hassan Baloch, Rahim Baksh na Imtiyaz Daryayi, kwa lengo la kubaini mmiliki wa shehena waliyopatikana nayo.
Inspekta Shadrack Kemei, aliomba siku 30 kufanya uchunguzi wa kimaabara na kukamilisha upelelezi.
“Mahakama hii inatakiwa kutoa amri inayoruhusu (polisi) kushikilia vifaa vya kielektroniki vilivyopatikana wakati wa kukamatwa, kwa madhumuni ya uchunguzi wa kimaabara,” alisema katika hati ya kiapo.
Mpelelezi huyo pia ameomba amri inayowalazimisha wageni hao kutoa misimbo yote ya kufungua simu hizo ili kuruhusu uchunguzi wa kimaabara kufanyika.
Washukiwa hao walikamatwa baada ya Jeshi la Wanamaji la Kenya kunasa chombo cha baharini ambacho hakikuwa na alama za utambulisho.
Chombo hicho kilipelekwa katika Bandari ya Kilindini mnamo Oktoba 24, ambapo maafisa, wakitumia kibali cha upekuzi kutoka Mahakama ya Mombasa, waligundua vifurushi 769 vyenye uzito wa kilo 1,035.986, vinavyoshukiwa kuwa dawa ya kulevya aina ya methamphetamine.