Harambee Starlets ina dakika 90 kufuzu WAFCON dhidi ya Gambia
HARAMBEE Starlets ina dakika 90 leo, kuandikisha historia ya kufuzu kwa Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Mabinti (WAFCON) 2026, baada ya miaka 10 bila mafanikio.
Timu hiyo itamenyana na wenyeji Gambia, katika mechi ya marudiano ya raundi ya mwisho ya kufuzu, Uwanjani Stade Lat Dior mjini Thies, Senegal, saa kumi jioni saa za Senegal (saa moja usiku saa za Kenya) leo.
Starlets iliishinda Gambia 3-1 katika mechi ya mkondo wa kwanza Ugani Nyayo Nairobi Ijumaa iliyopita na kuweka guu moja katika mashindano hayo yatakayoandaliwa nchini Morocco kuanzia Machi 17 hadi Aprili 3.
Mshambuliaji Fatuomata Kanteh wa Gambia alicheka na wavu wa kwanza mapema dakika ya pili, kabla ya washambuliaji wa Kenya Mwahalima Adam, Fasilah Adhiambo, na Sheylene Opisa kufunga kila mmoja dakika ya 12, 19, na dakika za nyongeza kipindi cha kwanza mtawalia.
Kinachohitajika kwa Starlets katika mechi hii, ni kuepuka kuruhusu zaidi ya mabao mawil. Lakini sare ya aina yoyote pia, itawapa tiketi ya kuzu moja kwa moja.
Kufuzu kwao ni muhimu kwani, wamekuwa nje ya mashindano haya kwa muongo mmoja baada ya kukosa kufuzu kwa mashindano ya 2018, 2022, na 2024.
Kwa upande mwingine, Gambia inayotoka Afrika Magharibi inatazamia kufuzu WAFCON kwa mara ya kwanza baada ya majaribio matatu (2018, 2022, na 2024) bila mafanikio.
Pande hizi mbili zinakutana kwa mara ya pili sasa, mechi ya kwanza ikiwa Ijumaa iliyopita. Starlets walifika hatua hii kwa kuishinda Tunisi
1-0 kwa jumla ya mabao huku Gambia wakiinyorosha Niger 4-1 mwezi Februari mwaka huu.
Timu zote ziliwasili Senegal Jumamosi jioni na zilipangwa kufanya mazoezi yao ya mwisho jana ugani Lat Dior.
Kocha wa Starlets Beldine Odemba huenda alisifanye mabidiliko mengi kutokana na kile kikosi ambacho kilianza Ijumaa iliyopita. Ikiwa hili litatokea, ataangazia sana mashambulizi ikilinganishwa kwamba, walipoteza nafasi nyingi za wazi.
Odemba alimwanzisha Lilian Awuor langoni, akilindwa na Lorine Ilavonga na Elizabeth Muteshi, na nahodha Ruth Ingosi. Enez Mango, Adam, Lavender Akinyi, na Martha Amnyolete walidhibiti safu ya kiungo, huku Elizabeth Wambui, Opisa, na Adhiambo wakiongoza mashambulizi.
Kwa upande wa Gambia almaarufu Scorpions, walilemewa pande zote mbili katika mashambulizi na safu ya mabeki ambao walitatizika kuwadhibiti washambuliaji wa Starlets.