Amerika yaonya raia wake dhidi ya fujo Tanzania
UBALOZI wa Amerika nchini Tanzania umetoa ilani ya kiusalama kwa raia wake huku ghasia zikiripotiwa kote nchini humo baada ya uchaguzi wa urais na ubunge kuanzia.
Kwenye taarifa Jumatano, Oktoba 29, 2025, ubalozi huo ulithibitisha kuwa maafisa wa usalama wanapambana na wanaozua fujo huku ukitaka Waamerika kuchukua tahadhari ili kujikinga na hatari.
“Kuna ripoti kwamba maandamano yanafanyika maeneo mbalimbali. Maafisa wa usalama wanachukua hatua. Maafisa wa serikali ya Amerika wanashauriwa kusalia ndani ya makazi yao,” taarifa hiyo ilieleza.
Ubalozi huo uliwashauriwa raia wa Amerika kujiepusha na waandamanaji, kujiepusha na umati, kusalia watulivu, kufuatia taarifa kuhusu matukio kupitia vyombo vya habari na kuwa waangalifu na yanayoendelea karibu na mahala walipo.
Maandamano na fujo zimeshuhudiwa Jumatano, siku ambayo jumla ya Watanzania milioni 37 walipaswa kujitokeza katika zoezi la kuchagua Rais na wabunge.
Fujo ziliripotiwa katika miji kadhaa, ikiwemo Dar es Salaam na Arusha.
Jijini Dar es Salama, waandamanaji walikabiliana na polisi waliojibu kwa kuwarushia vitoza machozi, risasi za chuma na maji ya kuwasha.
Ripoti zaeleza kuwa vituo kadhaa za kupigia kura zilitekezwa maeneo kadhaa huku angalau gari moja la polisi likiharibiwa na kisha kuchomwa.
Ilisemekana kuwa wananchi walikuwa wakilalamikia hatua ya serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan kufanikisha kuzikwa kwa wagombeaji wakuu wa urais kama vile Tundu Lissu wa chama kikuu cha upinzani, Chadema na mgombeaji wa chama cha ACT-Wazalendo Luhaga Mpina.
Katika mji wa Kagera, ambako watu 17 walikamatwa kabla ya upigaji kura kuanza, makabiliano yalichacha kati ya vijana na maafisa wa usalama.
Katika maeneo kadhaa ya kisiwa cha Zanzibar, waandamanaji waliharibu mabango ya chama tawala, Chama cha Mapinduzi (CCM) huku wakiimba nyimbo za kuikashifu serikali.
Ripoti zinasema kuwa wanajesha walijitokeza jijini Dar es Salama kwa magari ya kukinga risasi, huku ikisemekana waliingilia kati kukinga wananchi dhidi ya ukatili wa polisi.
Mnamo Aprili mwaka huu, Tume Huru ya Kitaifa ya Uchaguzi (INEC) ilizima chama cha Chadema kushiriki uchaguzi huo.
Baadaye kiongozi wake, Bw Lissu alikamatwa na kuzuiliwa gerezani kwa kosa la uhaini.
Hii ni baada ya mwanasiasa huyo kuendesha kampeni ya kuwasihi wananchi wasusie uchaguzi mkuu hadi Mageuzi yafanywe kulainisha mfumo wa uchaguzi. Bw Lissu aliidai tume ya uchaguzi inapandelea chama cha CCM.
Na mwishoni mwa Septemba mwaka huu, Bw Mpinga ambaye ni mgombeaji urais wa chama cha ACT Mzalendo, alizuiliwa kuwania tume ya INEC kwa kutotimiza taratibu fulani hitajika.
Wadadisi wanasema hii ndio maana, baada ya kuzimwa kwa wapinzani wakuu, raia wamekasirikia wakisema ni njama ya kufanikisha ushindi wa Rais Suluhu na chama chake, CCM.
Sababu ni kwamba wapinzani wake 16 wanatoka vyama vyenye ufuasi finyu.