Habari

Tanzania hakukaliki!

Na WAANDISHI WETU October 30th, 2025 Kusoma ni dakika: 3

HALI ya taharuki imeendelea kutanda Tanzania baada ya uchaguzi wa Jumatano Oktoba 28, 2025 huku serikali ikiagiza wafanyakazi kusalia nyumbani ghasia zikiendelea kwa siku ya pili.

Vifo viliripotiwa polisi walipokabili waandamanaji na mashirika ya kimataifa yakaonya kuwa hali inaweza kuzidi kuwa tete.

Polisi nchini humo walitumia vitoa machozi na risasi mnamo Alhamisi kuwatawanya waandamanaji waliorejea barabarani kwa ujasiri siku moja baada ya uchaguzi mkuu uliokumbwa na ghasia, mashahidi walisema.

Maandamano yalizuka katika jiji la kibiashara la Dar es Salaam na miji mingine Jumatano wakati wa upigaji kura, kufuatia kupigwa marufuku kwa wagombea wakuu wawili wa urais waliokuwa wapinzani wa Rais Samia Suluhu Hassan, pamoja na madai ya ongezeko la ukandamizaji wa serikali.

Polisi walitangaza kafyu ya kutotoka nje usiku jijini Dar es Salaam makao ya zaidi ya watu milioni saba baada ya majengo ya serikali na ya kibinafsi kuchomwa moto.

Huduma za intaneti zilizokatizwa wakati wa uchaguzi ilianza kurejea taratibu Alhamisi.

Mwanaharakati wa haki za binadamu Tito Magoti aliambia Reuters kuwa, alipokea taarifa za vifo vya angalau watu watano kutokana na maandamano hayo, huku duru za kidiplomasia zikisema kuwa watu wasiopungua 10 waliuawa jijini Dar es Salaam.

Serikali na polisi hawakujibu maombi ya maoni.

Shirika la Habari la Serikali, Tanzania Broadcasting Corporation (TBC), lilianza kutangaza matokeo ya awali yakionyesha Rais Hassan akiongoza kwa kura nyingi katika maeneo mbalimbali.

Mashahidi waliripoti maandamano katika mitaa kadhaa ya Dar es Salaam ambapo polisi walifyatua risasi na vitoa machozi.

Miji ya Arusha na Mwanza pia ilishuhudia maandamano yaliyotawanywa kwa nguvu.

Serikali ya Uingereza ilitangaza kuwa safari za kimataifa zilihairishwa kuingia na kutoka katika Uwanja wa Ndege wa Dar es Salaam, huku viwanja vya Arusha na Kilimanjaro vikifungwa.

Ghasia hizi zimezua mtihani kwa Rais Hassan, ambaye alisifiwa aliposhika madaraka mnamo 2021 kwa kulegeza masharti ya kisiasa yaliyokuwa yamekandamiza upinzani chini ya mtangulizi wake, John Magufuli.

Hata hivyo, katika miaka ya hivi karibuni, wanaharakati wa haki za binadamu wameishutumu serikali kwa visa vya watu kutoweka bila maelezo.

Serikali imesema watumishi wa umma wataendelea kufanya kazi kutoka nyumbani hadi Ijumaa, na ikawahimiza wananchi kukaa majumbani isipokuwa kwa dharura.

Chama kikuu cha upinzani CHADEMA, ambacho kilipigwa marufuku kushiriki uchaguzi baada ya kukataa kusaini kanuni za maadili, kilikuwa kimeitisha maandamano wakati wa uchaguzi huo.

Kiongozi wake Tundu Lissu anakabiliwa na mashtaka ya uhaini.Pia, tume ya uchaguzi ilimwondoa mgombea wa chama cha ACT-Wazalendo, hali iliyomwacha Rais Hassan kukabiliwa na vyama vidogo visivyo na ushawishi mkubwa.

Jana, maandamano yalizuka katika kituo cha mpakani cha Namanga, upande wa Tanzania, baada ya serikali ya nchi hiyo kuzima intaneti Jumatano.Polisi wa Tanzania walikabiliana nao kwa kuwarushia vitoza machozi ili kuwatawanya hali iliyopelekea baadhi yao kuvuka hadi upande wa Kenya na kuwasha moto barabarani.Waliungwa mkono na baadhi ya wafanyabiashara katika eneo hilo la mpakani.

Kuanzia asubuhi, wingu la vitoa machozi liligubika eneo linalokaribiana na afisi za forodha za Kenya hali iliyowafanya watu waliofika kusaka huduma kutoroka.

Huku wakiimba nyimbo za kukashifu serikali ya Tanzania, waliharibu mabango ya kampeni yenye picha za Rais Suluhu wakitaja uchaguzi wa Jumatano kama “mzaha.”

“Uchaguzi uliofanyika nyumbani kwetu sio halali; ni mzaha mtupu. Matokeo yamejulikana. Serikali inatumia vyombo vya dola kutunyamazisha,” akasema Bw Denis Chitunde, mfanyabiashara.

Jana, katibu wa Wizara ya Usalama wa Ndani Kenya Raymond Omollo aliwaonya watu wanaopanga kusababisha fujo katika mpaka wa Kenya na Tanzania kwamba watakabiliwa na mkono wa sheria.

Akiongea wakati ambapo taharuki ilitanda kufuatia maandamano yaliyokithiri nchini Tanzania, Dkt Omollo aliwataka Wakenya kusalia watulivu na kuwaruhusu maafisa wa usalama kupambana na masuala yanayoibuka kwa mujibu wa sheria.

“Singetaka kuongea kuhusu yale yanayofanyika Tanzania, lakini ninaweza kuzungumza kuhusu masuala ya usalama nchini Kenya. Nchini Kenya, tuko na sheria inayoongoza maandamano. Tufanye yale sheria inaruhusu,” akasema.

Dkt Omollo alisisitiza kuwa huku Kenya ikiheshimu uhuru wa Tanzania, vitendo vinavyohujumu usalama haswa karibu na mipaka yetu havitavumiliwa.

“Tunaamini kuwa kuna sheria inayoongoza wenzetu kule Tanzania. Watanzania ni majirani zetu na tunawakia kila la heri. Lakini, tutapambana na chochote kinachohujumu sheria upande wa Kenya,” akasema huku akitoa wito kwa Wakenya wasichukue sheria mikononi mwao.

Aliongeza kuwa maafisa wanaosimamia usalama katika mpaka wa Kenya wako na uwezo wa kushughulikia masuala ibuka ya kiusalama na biashara.

Dkt Omollo aliwaonya Wakenya wanaoishi maeneo ya mpaka wa Kenya na Tanzania, kutoshiriki katika maandamano yaliyochochewa na masuala yanayohusiana na uchaguzi mkuu uliofanyika Jumatano.

“Maafisa wetu wa polisi wako chonjo kupambana na visa vyovyote vya utovu wa usalama ambavyo huenda vikasababishwa na taharuki za kisiasa nchini Tanzania,” akasema.

Alitoa wito kwa wafanyabiashara kushirikiana na walinda usalama katika vituo vya mpakani kama vile Namanga na Lunga Lunga.

Kauli ya Dkt Omollo ilijiri baada ya video kusambazwa mitandaoni ikiwaonyesha Wakenya wakielezea kuwaunga mkono waandamanaji nchini Tanzania waliokuwa wakipinga kile walichokitaja kama utawala dhalimu wa Rais Samia Suluhu Hassan.

Dkt Omollo alikuwa akiongea katika Chuo cha Mafunzo ya Utawala Nchini (KSG), Mombasa, baada ya kuzuru kituo cha kufuatilia masuala ya usalama na biashara bandarini.