Habari

Matiang’i sasa naibu wa Uhuru – Jubilee

Na JUSTUS OCHIENG October 31st, 2025 Kusoma ni dakika: 2

CHAMA cha Jubilee kimemteua rasmi aliyekuwa Waziri wa Usalama wa Ndani, Dkt Fred Matiang’i, kuwa Naibu Kiongozi wake na kuunga mkono azma yake ya kugombea urais mwaka 2027, hatua inayochukuliwa kuwa ishara wazi ya kumrithisha chama hicho kutoka kwa Rais mstaafu Uhuru Kenyatta.

Tangazo hili, lililotolewa Alhamisi, Oktoba 30, 2025, baada ya mkutano wa Kamati Kuu ya Kitaifa (NEC) ulioongozwa na Bw Kenyatta, linamtosa Dkt Matiang’i ndani kabisa katika mchakato wa ufufuzi wa Jubilee na juhudi za kuunganisha vyama vya upinzani nchini baada ya kifo cha kiongozi wa ODM, Raila Odinga.

Afisa mmoja wa ngazi ya juu wa Jubilee aliambia waandishi wa habari kwamba kuteuliwa kwa Dkt Matiang’i kuwa Naibu Kiongozi wa chama kunamfanya kuwa kiongozi wa kweli wa chama hicho, kwa kuwa Rais mstaafu Uhuru Kenyatta hataendesha siasa za kila siku.

“Uhuru hawezi kuzunguka akitafuta kura au kuongoza kampeni. Muda wake umekwisha,” alisema afisa huyo.

“Mtu ambaye anaweza kuchukua jukumu hilo sasa ni Dkt Matiang’i. Uhuru bado ni kiongozi wetu kwa jina tu ila sasa mtu wa kutegemewa ni Matiang’i.”

Afisa huyo aliongeza kuwa kuungwa mkono kwa Dkt Matiang’i kunampa nafasi ya kisiasa ndani ya chama na katika Muungano wa Upinzani.

“Tumemkubali kama mgombeaji wetu wa urais. Sasa ana nafasi halali ambayo awali hakuwa nayo. Kwa kuungwa mkono hivi, yuko kwenye meza ambapo maamuzi makuu ya upinzani yatafanywa,” alieleza afisa huyo.

Mkutano wa NEC wa jana, ambao ulikuwa wa kwanza baada ya taifa kuingia kipindi cha majonzi baada ya kifo cha Odinga, pia uliamua kumteua Dkt Matiang’i kuwa mwakilishi rasmi wa Jubilee katika Muungano wa Upinzani; jukwaa jipya la kisiasa linalojumuisha aliyekuwa naibu rais Rigathi Gachagua.

Wengine walio katika muungano huo ni Kalonzo Musyoka (Wiper Patriotic Front), Martha Karua (People’s Liberation Party), Eugene Wamalwa (DAP-K) na Justin Muturi (Democratic Party).

Naibu Mwenyekiti wa Jubilee, David Murathe, aliwaambia wanahabari kwamba chama bado kiko ndani ya muungano wa upinzani.“Uhuru yupo katika Muungano wa Upinzani, ndipo tunapaswa kuwa. Tutaunga mkono mgombea wa urais wa muungano, hata iwapo hatakuwa Matiang’i. Lakini kwa sasa, tumempa chama mgombeaji na mgombea huyo ni Matiang’i,” alisema Bw Murathe.

Duru ndani ya chama zinasema hatua hii ni sehemu ya mpango makini wa mpito ndani ya Jubilee. Wadokezi wengi chamani wasema Bw Kenyatta, alishinikiza kuingizwa kwa Dkt Matiang’i kwenye ngazi ya juu ya chama, akimtaja kama “mtiifu, anayependa mabadiliko, na anayeweza kuongoza Kenya katika hatua mpya ya siasa za uaminifu.”

Rais mstaafu anadaiwa kujiandaa kupunguza usimamizi wa kila siku wa chama mwanzoni mwa 2026, akiandaa njia kwa Dkt Matiang’i kuchukua mamlaka kamili.Safari ya kisiasa ya Dkt Matiang’i imekuwa ni mchakato wa taratibu.

Baada ya kuondoka serikalini mwaka 2022, alibaki kimya, akijikita katika masuala ya kitaaluma na sekta ya binafsi.