Muturi alijiuzulu, korti yasema ikitupa kesi ya kupinga uteuzi wa Oduor kuwa Mwanasheria Mkuu
MAHAKAMA Kuu imetupilia mbali kesi iliyopinga uhalali wa uteuzi wa Dorcas Oduor kama Mwanasheria Mkuu wa Serikali na kuondolewa ofisini kwa mtangulizi wake, Justin Muturi, ikisema kuwa Bw Muturi alijiuzulu kwa hiari na mchakato wa kisheria ulifuatwa.
Mahakama ilisema kuwa waliowasilisha kesi walishindwa kuthibitisha madai kwamba Rais William Ruto alimdhalilisha kikatiba Bw Muturi kupitia Amri ya Rais mnamo Julai 2024.
Mahakama ilithibitisha msimamo wa serikali kwamba Bw Muturi alijiuzulu ili kurahisisha mabadiliko katika Baraza la Mawaziri, jambo lililofanya uteuzi wa Bi Oduor kuwa halali. Ilisema mchakato wa kisheria ulifuatwa katika kuondolewa kwa Bw Muturi na kuteuliwa kwa Bi Oduor.
Kuondolewa kwa Bw Muturi kulitokea wakati wa mabadiliko makubwa ya serikali baada ya maandamano ya kitaifa ya Gen-Z mnamo 2024.
Awali, Rebecca Miano (sasa Waziri wa Utalii) alitarajiwa kumrithi, lakini Rais Ruto baadaye alimchagua Bi Oduor, ambaye wakati huo alikuwa akihudumu katika Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (ODPP).
Kundi la walalamishi saba, likiongozwa na Dkt Magare Gikenyi, lilihoji kuwa kuondolewa kwa Bw Muturi kupitia hotuba ya rais iliyopeperushwa kwenye televisheni na Tangazo la Gazeti Rasmi ya Serikali Nambari 8440 kuliweka hatarini masharti ya kikatiba chini ya Kifungu cha 132 na Sheria ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu, zinazobainisha misingi ya kuondolewa kwa Mwanasheria Mkuu ambayo ni tabia mbaya, ukosefu wa uwezo, au ukosefu wa ufanisi.
Walidai kwamba “barua ya kujiuzulu ya Bw Muturi na tangazo la gazeti lililorekebishwa” ni uongo ulioandaliwa ili kuhalalisha mchakato haramu.
Kesi yao ilidai kwamba Rais Ruto alitumia nadharia ya enzi za ukoloni ambayo walisema haiko katika mfumo wa kikatiba wa sasa wa Kenya.
Hata hivyo, mahakama iliamua kuwa walilalamishi hawakutoa ushahidi wa kuaminika kupinga yaliyothibitishwa na Ofisi ya Rais, Tume ya Huduma za Umma na Bunge, yanayothibitisha kujiuzulu kwa Bw Muturi.
“Walalamishi wametaja taarifa za vyombo vya habari, lakini ushahidi wa kupinga uliotolewa na washtakiwa unaonyesha kuwa Bw Muturi hakufutwa kazi bali alijiuzulu ili kuruhusu kubadilishwa kwa Baraza la Mawaziri,” mahakama ilisema
Mahakama ilitegemea stakabadhi muhimu kama barua ya kujiuzulu ya Bw Muturi aliyowasilisha Julai 11, 2024 kwa Rais Ruto na Tangazo la Gazeti Nambari 8440 la Julai 12, 2024, lililosema wazi kuwa Rais “alikubali kujiuzulu kwake.”
Mahakama pia ilitegemea rekodi za Bunge zinazoonyesha Bw Muturi alihudhuria Kamati ya Uteuzi mnamo Agosti 4, 2024, akithibitisha alijiuzulu kwa hiari ili “kusaidia Rais kupanga upya Baraza la Mawaziri.”
“Kesi ya mlalamishi inategemea dhana tu. Tangazo la gazeti ni ushahidi, na hakuna thibitisho la uongo,” ilisema mahakama ikirejelea Kifungu cha 85 cha Sheria ya Ushahidi.
Ilisisitiza kuwa walilamishi walishindwa kutoa ushahidi wa kuaminika kupinga barua ya kujiuzulu.