Habari

Waziri afichua wizi bila jasho serikalini

Na ERIC MATARA November 5th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

SEKTA ya Utumishi wa Umma nchini Kenya inakabiliwa na ufisadi mkubwa wa mishahara unaosababisha serikali kupoteza mabilioni ya pesa kila mwaka, Waziri wa Utumishi wa Umma, Bw Geoffrey Ruku amefichua.

Akizungumza katika kongamano la 29 la Usimamizi wa Wafanyakazi lililoandaliwa na Taasisi ya Usimamizi wa Wafanyakazi (IHRM) katika hoteli ya Sawela, Naivasha, Bw Ruku alisema utumishi wa umma sasa umevamiwa na mitandao ya walaghai inayojumuisha maafisa wakuu serikalini.

Waziri huyo alisema ukaguzi wa hivi majuzi wa mifumo ya wafanyakazi katika sekta ya umma ulifichua wizi, njama na matumizi mabaya ya mfumo wa mishahara, ambapo baadhi ya watumishi waliotimiza umri wa kustaafu miaka kadhaa iliyopita bado wanalipwa mishahara na marupurupu kinyume cha sheria.

“Tumeona udanganyifu mkubwa, ikiwemo watumishi kutumia vyeti bandia kupandishwa vyeo, kubadilisha tarehe za kuzaliwa na wengine kulipwa marupurupu mara mbili,” alisema Bw Ruku.

Aliongeza kuwa baadhi ya maafisa wamekuwa wakiepuka kulipa kodi, hali inayosababishia serikali mabilioni ya pesa kila mwaka.

Ripoti za Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali na Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) zimeunga mkono matamshi hayo, zikifichua visa vya maafisa walioajiriwa baada ya kustaafu na wengine kuendeleza ajira zao kwa kutumia hila.

Ukaguzi maalum uliofanywa na Mkaguzi Mkuu, Dkt Nancy Gathungu, ulibaini kuwa Tume ya Utumishi wa Umma (PSC) iliwalipa watumishi watano waliostaafu jumla ya Sh25.7 milioni kwa mikataba batili kati ya Machi 2023 na Septemba 2024.

Wastaafu hao, waliokuwa maafisa wa Idara ya Utumishi wa Umma na Hazina ya Kitaifa, walilipwa hadi Sh460,000 kwa mwezi, kinyume na sera ya ajira serikalini.

Bw Ruku alisema uchunguzi unaendelea dhidi ya mamia ya watumishi wa umma, akiahidi hatua kali kwa wote watakaopatikana na hatia ya kuchochea wizi wa mishahara.

Ripoti za hivi karibuni za EACC na Tume ya Utumishi wa Umma (PSC) zinaonyesha kuwa zaidi ya watumishi 2,000 walitumia vyeti bandia kutoka vyuo vikuu vya humu nchini na nje, shule za upili na vyuo binafsi ili kupata ajira. Katika vyeti 53,000 vilivyokaguliwa, 1,280 vilibainika kuwa vya kughushi. Kwa kipindi cha miaka minne, EACC imechukua hatua na kurejesha Sh14.3 milioni, huku ikilenga kufuatilia zaidi ya Sh400 milioni.

Aidha, ukaguzi wa mishahara ya serikali za kaunti uliofanywa kufikia Juni 30, 2024, ulibaini kuwa wafanyakazi 406 bado walikuwa kazini baada ya kufikisha umri wa kustaafu wa miaka 60, jambo linalokiuka sheria. Mombasa iliongoza kwa watumishi 96, ikifuatiwa na Kisumu (79) na Nakuru (77), huku jumla ya watumishi hao wakilipwa Sh32 milioni katika kipindi cha ukaguzi.

Waziri Ruku alisema wizara yake inashirikiana na EACC, Idara ya Uchunguzi wa Jinai (DCI), Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (ODPP) na IHRM kufuatilia wizi wa mishahara na vyeti bandia.

“Tumeanzisha apu ili kusaidia kusafisha mifumo wa ajira,” alisema na kuonya kuwa wote watakaopatikana na hatia watafutwa kazi na kushtakiwa.

Aidha, amesisitiza utekelezaji wa mfumo wa pamoja wa habari za wafanyakazi (UHRIS) na kufuata umri wa kustaafu wa miaka 60, huku zaidi ya 43,000 watumishi wakitarajiwa kustaafu kufikia 2029 kufungua nafasi kwa vijana.

Kwa mujibu wa Waziri Ruku, kashfa hizi zimeharibu uteuzi wa watumishi kwa misingi ya ujuzi na sifa, na kuongeza mzigo wa mishahara na pensheni kwa serikali.