Habari

Kenya yasukuma Tanzania kuhusu usalama wa raia wake

Na MERCY SIMIYU November 7th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

KENYA imeitaka Tanzania kutoa majibu kuhusu hali ya raia wake waliojipata kwenye mzozo wa baada ya uchaguzi, huku ikishinikiza serikali ya nchi hiyo ihakikishe usalama wao na kuchukua hatua dhidi ya ukiukaji wa haki zao.

Haya yanajiri baada ya taarifa  kuongezeka kuwa Wakenya walio nchi hiyo jirani wanaishi kwa hofu na vitisho vya kunyanyaswa wakishukiwa kushiriki maandamano yaliyosababishwa na uchaguzi wa Oktoba 29 na matokeo yake.

Katika siku za hivi karibuni, familia za Wakenya zimeeleza hofu zao kuhusu usalama wa wapendwa wao walio Tanzania, huku ripoti zikionyesha baadhi ya raia hao wameuawa, wengine wakikosa kufahamika waliko au wakiwa hospitalini, na wengine wakizuiliwa na polisi.

Familia ya mmoja wa Wakenya ilitangaza Jumanne kuwa walikuwa na taarifa za kuaminika kuwa mwanao, mwalimu aliyefanya kazi Dar es Salaam, aliuawa, lakini hawakuweza kupata mwili wake.

Novemba 6, 2025, Mkuu wa Mawaziri wa Kenya na Waziri wa Masuala ya Kigeni Musalia Mudavadi pamoja na Waziri wa Masuala ya Kigeni wa Tanzania Mahmoud Thabit Kombo walifanya kikao ambapo Kenya ilitaka usalama wa raia wake.

“Wakati wa mazungumzo, tulisisitiza umuhimu wa kuhakikisha usalama wa raia wote wa kigeni, wakiwemo Wakenya, ambao wanachangia maendeleo ya uchumi wa Tanzania kupitia biashara halali na huduma za kitaalamu,” alisema Mudavadi. Alithibitisha ripoti za mauaji, kuzuiliwa na kunyanyaswa kwa Wakenya na maafisa wa Tanzania.

“Kuna matukio yaliyoripotiwa ambapo haki za Wakenya wengi zimekandamizwa, na kesi hizi zimeshushwa rasmi kwa serikali ya Tanzania,” aliongeza.