Opta yabashiri Arsenal itatwanga Sunderland, Man U itafinywa na Tottenham Jumamosi
KOMPYUTA mahiri ya Opta imetoa utabiri wake wa mechi za Ligi Kuu ya Uingereza za wikendi ya Novemba 8-9, 2025, huku viongozi Arsenal wakilenga kusalia salama juu ya jedwali.
Manchester United nao wanatarajiwa kuwa na kibarua kigumu dhidi ya wenyeji Tottenham katika mechi itakayofungua shughuli wikendi hii hapo Jumamosi saa tisa unusu alasiri.
Vijana wa kocha Mikel Arteta wana alama 25 baada ya michuano 10 ya kwanza. Wamefungua pengo la alama sita dhidi ya nambari mbili Manchester City.
Wanabunduki wa Arsenal wanaweza kuongeza mwanya huo hadi pointi tisa kabla ya City kucheza Jumapili.
Safari ya Arsenal kuelekea ugani Stadium of Light kuvaana na Sunderland ndiyo kivutio kikuu cha mipepetano ya Jumamosi, ambapo vijana wa Arteta wanatafuta kuendeleza rekodi yao bora ya ushindi wa mechi 10 mfululizo katika mashindano yote. Kompyuta ya Opta inawapa Arsenal nafasi ya ushindi ya asilimia 69.8. Ni ubashiri mkubwa zaidi wa ushindi wa ugenini wikendi hii. Opta inawapa Sunderland matumaini ya kuchapa Arsenal ya asilimia 13.5 pekee.
Sunderland, ambao wamerejea Ligi Kuu tangu 2016-2027, wamekuwa miongoni mwa timu zilizoshangaza msimu huu wa 2025-2026. Wamepanda hadi nafasi ya nne kutokana na mwenendo mzuri.
Hata hivyo, historia haipo upande wa Sunderland. Hawajashinda katika mechi zao 23 zilizopita dhidi ya timu zinazopatikana katika mduara wa nne-bora (wametoka sare mara saba na kupoteza michuano 16 dhidi ya wapinzani ndani ya nne-bora).
Arsenal, ambao walishinda Ligi Kuu mara ya mwisho msimu 2003-2004, nao hawajapoteza katika mechi 15 za ligi dhidi ya Sunderland. Wamelemea Sunderland mara 10 na kutoka sare mechi tano. Mara tatu pekee ambazo Sunderland walichabanga Arsenal kwenye Ligi Kuu ilikuwa nyumbani kwao, zote kwa bao 1–0. Mara ya mwisho Sunderland walilemea Arsenal ligini ilikuwa 1-0 mwezi Novemba 2009.
Nahodha wa zamani wa Arsenal, Granit Xhaka, ambaye sasa ni nahodha wa Sunderland, anatarajia kuvunja rekodi hiyo baada ya kufunga bao lake la kwanza kwa klabu hiyo katika sare ya 1-1 na Everton hapo Novemba 3.
Kwa upande wa Arteta, jambo muhimu ni kudumisha umakini, huku wakibeba majukumu ya ligi na mashindano ya Ulaya.
Arsenal ndiyo timu pekee haijapoteza mchezo wowote kwenye Klabu Bingwa Ulaya tangu msimu uanze, wakionyesha uimara wa ulinzi na ukali wa mashambulizi.
Ushindi utawafanya Arsenal wapate uongozi wa alama tisa, na hivyo kuongeza shinikizo kwa City kabla ya mechi yao dhidi ya Liverpool hapo Jumapili.
City wamepewa nafasi ya asilimia 45.4 kushinda, huku Liverpool wakiwa na asilimia 27.7. Uwezekano was are kupatikana ni asilimia 26.9.
Matokeo ya mchuano huo yanaweza kubadilisha mwelekeo wa vita vya ubingwa.
Macho yatakuwa kwa Xhaka na mfumaji matata Wilson Isidor kambini mwa Sunderland, na beki Gabriel Magalhaes na mshambulizi wa dharura Mikel Merino (Arsenal).
Kwingineko, Chelsea ndio chaguo la kuaminika zaidi la kompyuta ya Opta, wakiwa na nafasi ya asilimia 73.2 ya kucharaza Wolves, matokeo yanayoweza kumsaidia Arteta anapotazama ratiba ya Desemba. Wakati huo huo, Aston Villa (asilimia 49.9) na West Ham (asilimia 47.9) wanabashiriwa kutamba nyumbani, huku Everton (asilimia 45.8) wakitarajiwa kurejea katika hali nzuri dhidi ya Fulham.
Arsenal wamekuwa hatari zaidi ugenini, wakivuna alama 14 kati ya 18 zilizowezekana. Arteta ametilia mkazo katika kubadilisha wachezaji ili kudumisha nguvu, akiwapa nafasi vijana kama Ethan Nwaneri na Reuell Walters. Mtindo wa Arsenal wa presha ya juu, kasi ya mashambulizi, na ufanisi wa kumalizia umefanya timu hiyo kuwa kamili zaidi msimu huu wa ligi.
Ingawa mechi dhidi ya Sunderland inaonekana rahisi, Arteta amewaonya wachezaji wake wasijisahau. “Lazima tuheshimu kila mpinzani. Sunderland ni wagumu na wanajiamini sana nyumbani kwao,” akasema.
Iwapo Arsenal watashinda na City kupoteza mikononi mwa Liverpool, wanabunduki wataingia mapumziko ya kimataifa ya Novemba wakiwa kileleni kwa tofauti kubwa ya pointi. Hiyo itakuwa faida ya kisaikolojia kuelekea nusu ya pili ya msimu. Wakiwa na kina cha kikosi, uimara na ari, Arsenal wanaonekana wako tayari kuendeleza safari yao ya ubingwa.
Kadri kompyuta ya Opta inavyobashiri wikendi nyingine yenye msisimko wa Ligi Kuu, macho yote yatakuwa kwa viongozi kutoka Kaskazini mwa London, timu ambayo imejifunza tena sanaa ya kushinda kwa nidhamu, kujiamini na ubora.
Hata hivyo, mchuano kati ya Tottenham na mashetani wekundu wa United pia inatarajiwa kusisimua. Wenyeji Tottenham wanapigiwa upatu kutwanga United ama kutoka sare.
Opta imewapa Tottenham asilimia 47.5 ya kutwaa ushindi nyumbani dhidi ya United, kutoka sare asilimia 26.1 na kupoteza aslimia 26.4. Washambulizi Richarlison (Tottenham) na Bryan Mbeumo (Manchester United) watakuwa mstari wa mbele kutafutia klabu zao mabao.