Ugonjwa haupigi hodi, hivyo mjipange mapema
WANANDOA wengi hupanga mambo mengi; kuanzisha biashara, kununua nyumba, au kuwekeza katika elimu ya watoto.
Lakini jambo moja ambalo wanandoa wengi husahau kulipangia ni afya.
Baadhi hugutuka pale ambapo ugonjwa unapoingia ghafla, bila maandalizi ya kifedha au kihisia.
Kulingana na mshauri wa masuala ya ndoa na familia, Charity Phoebe, ugonjwa ndani ya ndoa unaweza kujaribu uhusiano zaidi ya changamoto nyingine yoyote.
“Mume au mke anapougua katika ndoa, hasa kwa muda mrefu, mzigo wa kifedha, kihisia na hata kimwili huwa mkubwa. Bila maandalizi, hali hiyo inaweza kusababisha migogoro na hata talaka,” anasema Bi Charity.
Mtaalamu huyo anashauri kwamba kupanga masuala ya afya mapema ni muhimu kama vile tu ilivyo kupanga bajeti ya chakula au kodi ya nyumba.
Hii ni pamoja na kuwa na bima ya afya, kuweka akiba ya dharura na kujadili namna ya kushughulikia matibabu iwapo mmoja atapata ugonjwa wa muda mrefu.
“Mipango ya afya haimaanishi unatarajia maradhi. Ni hekima. Hata vijana wenye afya njema wanapaswa kujadili kuhusu bima ya matibabu, hospitali wanazopendelea, na nani atahudumia watoto endapo mmoja atalazwa,” anaongeza Bi. Okello.
Naye mtaalamu wa masuala ya fedha Samuel Ochieng, anasema kuwa ugonjwa usiopangwa unaweza kuharibu kabisa mipango ya kifedha ya familia.
“Watu wengi hutumia akiba zote, kuuza mali au kukopa pesa kwa riba kubwa ili kugharamia matibabu. Hali hii inaweza kuzua lawama, msongo wa mawazo na hata kufikia talaka.”
Wanandoa pia wanahimizwa kuwa na mazungumzo ya wazi kuhusu afya zao.
Kuficha maradhi au kupuuzia dalili kunaweza kufanya mambo kuwa mabaya zaidi.
“Uaminifu kuhusu afya ni sehemu ya uaminifu wa ndoa. Ni lazima muwe na uhusiano wa kusaidiana badala ya kulaumiana,” asema Bi. Okello.
Kwa hivyo, kama mnavyopanga likizo, ada za shule au uwekezaji, panga pia afya yenu.
Ugonjwa haupigi hodi, lakini maandalizi mazuri yanaweza kuokoa ndoa, maisha na amani ya familia.
Kulingana na washauri hao, wanandoa wanaweza kuanza kwa hatua ndogo kama kuchangia mfuko wa afya wa familia kila mwezi, kujua vituo vya afya vilivyo karibu, na kujifunza kuhusu lishe bora na mtindo wa maisha unaoimarisha kinga ya mwili. “Hayo yote yakifanywa kwa umoja, yataimarisha si tu afya bali pia uhusiano wenyewe. Hivyo, anzeni kuangia afya yenu mapema,’ anasea Bi Charity.