Habari

Asimulia alivyotishwa kwa kuanika mauaji Shakahola

Na BRIAN OCHARO November 12th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

ALIYEKUWA mfuasi wa Pasta Paul Mackenzie amechua alivyoonya kuhusu mauaji ya Shakahola.

“Nilichoshwa na mafundisho tata ya pasta Paul Mackenzie kuhusu mwisho wa dunia. Niliona maafa yakija.”

Hayo yalikuwa maneno ya Bi Brenda Mwaura, aliyekuwa mshiriki wa kanisa la Good News International (GNI) na mfuasi wa mhubiri huyo, alipofika kutoa ushahidi mbele ya mahakama ya Mombasa jana.

Bi Mwaura, ambaye sasa anajulikana kama mlalamishi mkuu katika kesi hiyo, hakuwa mshiriki wa kawaida bali alikuwa mhusika muhimu katika kurekodi, kuhariri na kusambaza mahubiri ya Mackenzie kupitia kituo cha Times TV kwa mauzo kwa waumini na watu wengine waliovutiwa na mafundisho yake.

Katika chapisho lake la Facebook mwezi Novemba 2022, miezi minne tu kabla ya mauaji ya Shakahola kufichuliwa, alidai kuwa Mackenzie alikuwa “akiwaua watu na kuwazika kwenye shamba lake.” Alimtaja pia Mkurugenzi wa Uchunguzi wa Jinai (DCI) akitaka achukue hatua, lakini hakuna kilichofanywa.

“Sipuuza onyo hilo. Nilipata habari kutoka kwa baba yangu kwamba watu walikuwa wanakufa kule shambani. Aliniambia Mackenzie anaua watu na hakuna alikuwa akisaidia. Watu hawakuruhusiwa kuondoka,” alisema Bi Mwaura.

Baba yake, ambaye alikuwa mhubiri wa zamani wa GNI na pia alikuwa akisafirisha maua kutoka Nairobi hadi Shakahola, alikosana na Mackenzie kutokana na tofauti za kiimani.

Siku iliyofuata, chapisho hilo lilikuwa limeondolewa. Hii ilikuwa baada ya Mackenzie kutembelea ofisi za DCI mjini Malindi, akitaka msaada wa kuwatambua, kuwakamata na kuchukua hatua za kisheria dhidi ya mwandishi wa chapisho hilo.

“Nilichopata tu ni vitisho kutoka kwa watu wa Mackenzie,” alisema.

Watu wawili walimpigia simu wakimtisha. “Waliniambia sijui nilichokuwa nikichapisha na kwamba wangenifuata,” alisema. Alisema hakujitokeza kwa polisi kwa hofu ya kutowekwa kizuizini au kutoweka kwa nguvu.

Kulingana na shahidi huyo, mmoja wa waliompigia simu alikuwa mshiriki wa kanisa la Good News International (GNI) ambaye alikuwa akiunganisha Mackenzie na ulimwengu wa nje, akimjulisha kuhusu shughuli za mitandaoni.

“Sikuitikia wito wa polisi kwa sababu niliogopa huenda ningekuwa mhanga wa kuwekwa kizuizini au kupotea,” aliongeza Bi Mwaura.

Akihojiwa na wakili wa Mackenzie, Bi Mwaura alisema baba yake alijiondoa kanisa laMackenzie “alipoanza kuwaua watu,” akiongeza: “Alikuwa anatoa maagizo kwa wafuasi wake watekeleze ‘kazi hiyo’ kwa niaba yake.”

Akitoa ushahidi kupitia video mbele ya Mahakama ya Mombasa, ambako Mackenzie na washukiwa wengine 95 wanakabiliwa na mashtaka 238 ya mauaji, Bi Mwaura alieleza jinsi alivyojiunga na kanisa hilo akiwa na umri wa miaka 14.

“Familia nzima tulihudhuria tawi la GNI Makongeni, Nairobi. Tulifundishwa kuwa kazi, elimu, dawa za hospitali na vipodozi ni dhambi na kinyume na mapenzi ya Mungu,” alisema.

Alisema mafundisho yao yalilenga “kujiandaa kwa kurudi kwa Yesu Kristo” na kwamba walipaswa kuishi maisha safi. Mwaka huo huo, aliacha shule na hakufika Kidato cha Pili.

“Nilikuwa na miaka 14 pekee. Kama ningechapwa, ningerudi shuleni,” alisema huku akionyesha majuto.

Baadaye, Mackenzie alitumia mfano wake katika mahubiri dhidi ya elimu, akisema, “Brenda aliacha shule na sasa ndiye mhariri wa video katika Times TV.”

Baada ya muda, Bi Mwaura alianza kuchoshwa na mafundisho hayo. “Nilikua mtu mzima na nikachoka na ujumbe wa upuuzi kuhusu mwisho wa dunia. Hapo ndipo nilipoamua kuondoka,” alisema.

Aliongeza kuwa wakati wa janga la COVID-19, Mackenzie aliuza vifaa vya kanisa vilivyonunuliwa na waumini. “Alisema hakukuwa na kanisa tena. Hata gari alilouza lilikuwa la kanisa,” alisema.