Habari

Kenya yaangukia dhahabu ya mabilioni

Na PATRICK ALUSHALA November 12th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

KAMPUNI ya Uingereza, Shanta Gold Kenya Limited, inapanga kuwekeza Sh26.86 bilioni kwa uchimbaji wa dhahabu katika Kaunti ya Kakamega.

Madini hayo yamekadiriwa kuwa na thamani ya takribani Sh683.04 bilioni.

Taarifa hiyo imebainishwa katika ripoti ya tathmini ya athari kwa mazingira (EIA) ambayo kampuni hiyo imewasilisha kwa Mamlaka ya Kitaifa ya Usimamizi wa Mazingira (Nema), ikiomba idhini ya kuanzisha mgodi wa dhahabu na kituo cha usindikaji katika eneo la Isulu-Bushiangala, Kaunti ya Kakamega, kwa kipindi cha miaka minane.

Shanta Gold Kenya Limited ni tawi la kampuni mama Shanta Gold, iliyosajiliwa Guernsey, Uingereza, na ambayo pia inaendesha shughuli za uchimbaji madini hayo nchini Tanzania.

Mradi wa Isulu-Bushiangala ni sehemu saba za utafiti wa madini zinazojulikana kama “Mradi wa Magharibi mwa Kenya”, zinazohusisha kaunti kadhaa za magharibi mwa Kenya.

 Mwezi Oktoba, kampuni hiyo ilithibitisha kuwa imeomba idhini ya Nema kuanzisha mradi mwingine wa uchimbaji wenye thamani ya dola milioni 137 (Sh17.7 bilioni) katika maeneo ya Ramula (Siaya), East Gem, na Mwibona (Vihiga).

Kampuni hiyo inakadiria kwamba maeneo ya Isulu na Bushiangala katika eneo bunge la Ikolomani yatatoa takribani wakia 1,270,380 za dhahabu ya ubora wa juu sana.

“Madini ya dhahabu katika maeneo ya Isulu na Bushiangala yapo ndani ya miamba yenye ufa, iliyozungukwa na mawe ya volkeno na mchanga wa aina tofauti,” kampuni ilieleza.

Ukanda wa dhahabu wa Kakamega una historia ndefu tangu miaka ya 1930, ambapo wachimbaji wa kikoloni walianzisha migodi ya kwanza ya kibiashara nchini. Jina Ikolomani linatokana na neno la Kiluhya “okhooloma” likimaanisha mgodi wa dhahabu.

Kwa sasa, wakia moja ya dhahabu inauzwa kwa wastani wa dola 4,111.39 (takribani Sh530,985), na hivyo madini ya Kakamega yanakadiriwa kuwa na thamani ya Sh683.04 bilioni, sawa na mara 2.3 ya thamani ya uchumi wa kaunti hiyo. Kitaifa, thamani hiyo ni takribani asilimia 4.1 ya Pato la Taifa (GDP) la jumla ya Sh16.22 trilioni.

Shanta inatarajia kulipa mirahaba ya kati ya dola milioni 4.3 (Sh555 milioni) na dola milioni 4.7 (Sh607 milioni) kwa mwaka, pamoja na kodi ya Maendeleo ya Madini ya takribani dola milioni 1.5 (Sh193.7 milioni) kila mwaka.

Kaunti ya Kakamega itapokea asilimia 20 ya mapato ya miraha, huku jamii za wenyeji zikipewa asilimia 10, ambazo ni takribani Sh11 milioni na Sh5.5 milioni kwa mwaka wa uchimbaji.

Zaidi, kampuni hiyo italazimika kuwa na makubaliano rasmi na jamii zilizoko eneo la mradi na kugawa asilimia moja ya thamani ya dhahabu itakayozalishwa ambayo ni takribani Sh6.83 bilioni kwa kipindi cha miaka saba.

“Mradi huu unalenga kupata idhini ya kuchimba dhahabu kwa manufaa ya kiuchumi, na unatarajiwa kuchochea ukuaji wa uchumi wa eneo hilo kupitia ajira, biashara, na mapato ya serikali,” kampuni ilisema.

Kulingana na Wizara ya Madini, mradi wa Shanta unaweza kuwa mabadiliko makubwa katika sekta ya madini nchini Kenya, ambayo kwa muda mrefu imekuwa ikichechemea licha ya kuwa na utajiri wa madini. Serikali hivi karibuni ilipunguza mirahaba kutoka asilimia 5 hadi 3, ili kuvutia wawekezaji wakubwa.

Kwa muda mrefu, uchimbaji wa dhahabu nchini umekuwa ukifanywa kwa kiwango kidogo na kwa njia zisizo rasmi, ambazo zinahusisha hatari kama matumizi ya zebaki, mazingira hatari, na ajira za watoto, hali inayoathiri mapato ya wachimbaji na serikali.

Mapato ya Kenya kutokana na dhahabu yameshuka kwa miaka miwili mfululizo kufikia Sh3.02 bilioni mwaka 2024, kutoka Sh3.18 bilioni mwaka uliotangulia na ya juu zaidi kupatikana ya Sh3.38 bilioni mwaka 2023, kulingana na Ripoti ya Kiuchumi ya 2024.

Kampuni hiyo inapanga kununua takribani hekari 337 za ardhi, nyingi zikiwa mashamba ya watu binafsi, jambo litakalosababisha familia 800 kuhamishwa. Tayari imebaini maeneo sita inayoweza kuwahamishia, ya ukubwa wa hadi hekari 1,932, ambapo wakazi watachagua kati ya fidia ya fedha taslimu au makazi mapya ndani ya eneo hilo.