Makala

Siku za mwisho za mwanamuziki wa injili Betty Bayo

Na ELIZABETH NGIGI November 12th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

MWANAMUZIKI maarufu wa injili Betty Bayo, jina kamili Beatrice Mbugua, alijulikana kwa tabasamu lake ang’avu, nyimbo zenye kuinua mioyo, na utu wake wa upendo uliowagusa maelfu ya watu.

Lakini hata baada ya kugunduliwa  alikuwa akiugua leukemia,Betty aliendelea kuficha maumivu yake nyuma ya tabasamu hilo. Aliwaomba marafiki zake wa karibu na familia wasifichue kwamba alikuwa mgonjwa.

Marafiki zake wanasema alihofia kuwa katika hali yake dhaifu, wana mitandao wangeanza kumkejeli,  hasa kutokana na misukosuko aliyowahi kupitia mitandaoni hapo awali.

Mary Wanjiru, anayejulikana kwa jina maarufu Shiro wa GP, ambaye ni rafiki wa karibu na pia mwanamuziki wa injili, ndiye aliyekuwa naye katika wiki zake za mwisho zilizojaa uchungu mwingi.

Katika mahojiano maalum na Taifa Leo Shiro alisema ugonjwa wa Betty ulianza ghafla. Dalili za kwanza zilijitokeza katikati ya Oktoba, alipokuwa akionekana kuchoka kupita kiasi, kukaa kimya, na mara nyingi kukosa nguvu.

“Tulipokutana mara kadhaa, Betty alionekana mnyonge na mwenye uchovu,” Shiro anakumbuka. “Alikataa kuendesha gari tena na mara nyingine alikuwa analala katikati ya mikutano yetu.”

Mnamo Oktoba 18, Betty alimwambia Shiro kuwa alikuwa akihisi vibaya. Walienda katika Hospitali ya RFH, ambako madaktari walibaini alikuwa na kiwango cha chini cha damu na alikuwa akivuja damu kupita kiasi. Awali walidhani ni hedhi, lakini dalili za kizunguzungu na kuchoka ziliwatia wasiwasi.

Alilazwa hospitalini kwa siku tano na kuongezewa damu lakini madaktari walihitaji kufanya vipimo zaidi.

“Siku ya pili hospitalini, aliniita akiwa na mumewe Hiram. Walikuwa wamepata ripoti kwamba alikuwa akiugua leukemia,” Shiro anasema.

Familia ilishauriwa kumpeleka katika Hospitali ya Aga Khan kwa matibabu maalum. Kwa kuwa mumewe Hiram Gitau (Tosh) anaishi Amerika, familia ilipanga asafiri kwenda huko kwa matibabu zaidi.

Lakini Betty hakuamini alichokuwa akisikia.“Alisema hawezi kuwa mgonjwa kwa kiwango hicho,” Shiro alieleza. “Mumewe alirudi Amerika huku sisi tukipanga safari yake ya matibabu.”

Mnamo Oktoba 27, hali yake ilianza kuzorota zaidi, na alirudishwa RFH baada ya damu aliyokuwa ameongezewa kumalizika. Marafiki walilazimika kumshawishi akubali matibabu, na wakafungua kundi la WhatsApp la watu takriban 30 kumpa moyo.

Kila alipoongezewa damu, alikuwa akipata nguvu kidogo na kuomba kurudi nyumbani. Shiro alimwita tena Hiram kumwomba arejee nyumbani ili waandamane naye kwenda akapate matibabu. Kufikia wakati huo Betty alikuwa akivuja damu sana na hatimaye alikubali kupambana na ugonjwa huo. Novemba 3, alilazwa katika Hospitali ya AAR.

Baada ya siku mbili, afya yake ilidhoofika ghafla.
Alipata kiharusi (stroke) kutokana na kutokwa damu ndani kwa ndani, ingawa madaktari waliweza kuzuia hali hiyo, lakini Betty akapoteza uwezo wa kuzungumza.

Madaktari wa AAR walishauri apelekwe Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta (KNH), katika wodi ya wagonjwa binafsi kwa matibabu maalum zaidi.

Wakati wote huo, Betty aliomba hali yake ibaki siri.

“Aliomba tusiposti picha zake wala kuanzisha michango mtandaoni,” Shiro anasema. “Alisema amepigana vita vingi mtandaoni na hataki kutukanwa katika udhaifu wake.”

Hata akiwa katika maumivu makali, aliendelea kulinda heshima yake.

“Alisema watu wanapaswa kufa wakiwa na heshima zao,” Shiro anasema kwa uchungu.

Siku yake ya mwisho kabla hajapoteza sauti kabisa, aliimba wimbo wake alioupenda zaidi — ‘11th Hour.’

Kabla ya kuhamishiwa KNH, watoto wake wawili waliletwa kumuona.

“Hakuweza kuzungumza. Alipowaona watoto wake, alianza tu kulia,” Shiro anakumbuka.

Madaktari walibaini mwili wake ulikuwa unakataa damu mpya aliyokuwa akiwekwa, ishara kwamba alikuwa katika hatua ya mwisho ya ugonjwa huo.

Asubuhi ya siku aliyofariki, wanasaikolojia wa KNH walikaa na watoto wake kuwaandaa kupokea habari hizo.

“Walilia walipomwona mama yao na wakaahidi watakuwa watoto wema,” Shiro alisema.

Betty alifariki Jumatatu, Novemba 10, mwili wake ukiwa umedhoofika kupita kiasi kwa kupambana zaidi.
Ameacha watoto wawili na urithi wa muziki wa injili uliowafariji na kuinua maelfu ya watu.

Maandalizi ya mazishi yanaendelea, wasanii na marafiki wanakutana kila siku kuanzia saa 12 jioni katika Hoteli ya Bluesprings na nyumbani kwake EdenVille Estate, Barabara ya Kiambu.