Ruto aambia majaji kutotegemea AI kutoa uamuzi
RAIS William Ruto amewaonya majaji dhidi ya kutegemea Akili Unde (AI) katika maamuzi ya masuala ya wakimbizi na uhamiaji, akisema mifumo hiyo inaweza kuhatarisha usawa na utu katika mchakato wa kuomba hifadhi.
Akielezea mwelekeo wa Kenya katika usimamizi wa uhamiaji, Rais alikiri kwamba AI inaweza kurahisisha taratibu, lakini akasisitiza kuwa teknolojia lazima ibaki chini ya mamlaka ya maamuzi ya kibinadamu.
Alizungumza Novemba 17, 2025 wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa 14 wa Kimataifa wa Chama cha Majaji wa Wakimbizi na Uhamiaji (IARMJ) jijini Nairobi.
“AI inaweza kusaidia kupunguza msongamano wa kesi na kuongeza upatikanaji wa haki, lakini kutegemea kupita kiasi mifumo ya aina hii kunaweza kuathiri usawa,” alisema Rais Ruto mbele ya mamia ya majaji kutoka sehemu mbalimbali za dunia. “Teknolojia lazima iwe mtumishi wa haki, si mtawala wake.”
Rais alionya kuwa utoaji wa maamuzi bila uwazi na ukosefu wa uelewa wa muktadha ni hatari kubwa katika kesi za wakimbizi. Alisema kuwa ulinzi wa wakimbizi unahusisha utu na ubinadamu kipengele ambacho mashine haziwezi kuiga, na hivyo matumizi ya AI yanapaswa kuambatana na uwazi, uwajibikaji na usimamizi wa mahakama.
Ruto alithibitisha kujitolea kwa Kenya kulinda haki za wakimbizi, akisema kuwa nchi inahifadhi karibu wakimbizi 580,000, mojawapo ya idadi kubwa zaidi duniani. Alitaja pia utiifu wa Kenya kwa mikataba ya kimataifa kama Mkataba wa Wakimbizi wa UN wa 1951, Mkataba wa OAU wa 1969, na Sheria ya Wakimbizi ya 2021 ambazo alisema kuwa “ya kisasa na ya kuendeleza haki,” kwa kuwa inawapa wakimbizi haki ya kufanya kazi, kusafiri na kulindwa dhidi ya kurejeshwa makwao kwa nguvu.
“Kama sera yetu ya kufungua milango inaonyesha moyo wetu, basi utawala wa sheria ndio uti wa mgongo tunaoweka imara,” alisema.
Mapema mwaka huu, Kenya ilizindua mpango unaobadilisha kambi za wakimbizi kuwa makazi jumuishi ambapo wakimbizi na jamii zinazowahifadhi wanaishi na kushirikiana kiuchumi. Mpango huo unaendana na Mkataba wa Kimataifa wa Wakimbizi na msukumo wa Afrika wa suluhu za kujitegemea.
Rais alisisitiza umuhimu wa majaji kulinda haki za wakimbizi na kuratibu tafsiri za sheria za kimataifa katika mahakama mbalimbali.