Kauli za Tutam zatanda bungeni, wabunge wakichangamkia Hotuba ya Rais Ruto
RAIS William Ruto Alhamisi, Novemba 20, 2025 alilazimika kukatiza, kwa muda hotuba yake, baada ya wabunge kulipuka kwa kutoa kauli za “Tutam”!, “Tutam”!, yaani apaswa kuhudumu muhula wa pili.
Wengine walitoa kauli za “Fire! Fire! Fire!” (moto, moto, moto) wakati Dkt Ruto alikuwa akielezea mipango ya serikali yake ya kupanua miundo msingi ya barabara.
Rais alielezea mpango wa serikali yake kuanzisha ujenzi wa barabara kuu ya Rironi-Mau Summit, mradi ambao Dkt Ruto atazindua Ijumaa, Novemba 21, 2025.
“Kuanzishwa kwa mradi huu, kutapunguza msongamano katika barabara kuu ya kutoka Nairobi hadi Nakuru na Mau Summit.
Madereva wamekuwa wakipata hasara kubwa katika barabara hii kutokana na msongamano wa kila mara, kero ambalo sasa halitakuwepo mradi huo utakapokamilika 2027,” Dkt Ruto akaeleza.
Kiongozi wa taifa pia aliorodhesha barabara kadhaa kuu nchini ambazo zitapanuliwa kuwa zenye safu mbili, mojawapo ya barabara hizo ikiwa ni ile ya kutoka Kisumu hadi Busia.
Dkt Ruto pia alielezea ufanisi wa serikali yake katika sekta za Elimu, Afya, Kilimo, Kawi na uchukuzi ambao umeleta manufaa kwa raia wa taifa.
Seneta wa Bomet Hillary Sigei aliunga mkono hatua ya wabunge kutoa kauli za “Tutam” bungeni akisema wabunge hawakuvunja kanuni zozote za bunge.
“Bunge ni asasi ya siasa kwa hivyo ilikuwa sawa kwa wabunge kuchangamkia mipango ambayo serikali ya Rais William Ruto ametekeleza na ile ambayo anapania kutekeleza siku za usoni. Kwa hivyo, kwa mtazamo wangu ni sawa kwa wabunge kufurahia mipango hiyo na kupendekeza kuwa anafaa kupewa muhula mwingine afisini,” akaeleza seneta huyo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Seneti kuhusu Haki, Masuala ya Kisheria na Haki za Kibinadamu.
Mbunge wa Gem Elisha Odhiambo pia aliunga mkono Hotuba ya Rais Ruto akisema ulishehemu mipango mizuri ambayo itachochea ukuaji wa kiuchumi nchini.
“Kwa mfano, nilifurahishwa na Rais Ruto alipoelezea nguzo nne ambazo serikali yake itazipa kipaumbele kuiwezesha nchi hii kupiga hatua kimaendeleo. Hizo ni; Uwekezaji katika Elimu na ubunifu, kupigwa jeki kwa uzalishaji wa chakula kupitia kilimo cha unyunyiziaji, ustawishaji wa sekta ya kawi na uimarishaji wa sekta ya uchukuzi,” akasema Mbunge huyo anayehudumu muhula wa pili.
Wabunge wengine waliochangamkia hotuba ya Rais Ruto ni Charity Gathambi (Njoro) na John Waluke (Sirisia).
Hata hivyo, Mbunge wa Mavoko John Makau alitofautiana na wenzake akitaja hotuba ya Rais Ruto kama “wenye makisio mengi bila mpango madhubutu ya utekelezaji”.
“Inasikitisha kuwa Rais Ruto alitangaza mipango mikubwa ya ujenzi wa aina mbalimbali ya miundo msingi kama vile barabara itakayogharimu fedha nyingi zaidi hali inaashiria kuwa raia bado watabebeshwa mzigo mkubwa wa ushuru,” akaeleza Mbunge huyo wa chama cha Wiper Patriotic Front (WPF).
Kulingana na Bw Makau Hazina ya Kitaifa ya Miundo Msingi (NIF) ambayo serikali inalenga kubuni ili kufadhili miradi hiyo bado itagharamiwa na fedha za umma, zitakazopatikana kutokana na utozaji ushuru.