Kimataifa

Japan yaonya raia wake uhasama na China kuhusu Taiwan ukitokota

Na REUTERS November 19th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

TOKYO, JAPAN

JAPAN imewaonya raia wake wanaoishi China wahakikishe usalama wao na wajizuie kufika kwenye maeneo yenye watu wengi huku uhasama wa kidiplomasia kati ya nchi hizo mbili ukiendelea kutokota.

Nchi hizo mbili zenye uchumi mkubwa ukanda wa Asia zimetifuana kutokana na matamshi ya Waziri Mkuu wa Japan Sanae Takaichi kuhusu Taiwan.
Takaichi aliwaambia wabunge wa Japan kuwa iwapo China itavamia Taiwan, basi nao watalazimika kutumia majeshi yao kuingia vitani dhidi ya China.
Jana, afisa wa ngazi ya juu katika serikali ya Japan alikutana na mwenzake wa China jijini Beijing ili kujaribu kuzima taharuki hiyo inayonukia lakini hakukuwa na mwafaka wowote.
Wizara ya Masuala ya Kigeni ya China ilisema kwamba ilikuwa ikishinikiza Takaichi aombe msamaha kuhusu kauli yake. Hata hivyo, Msemaji wa Serikali ya Japan Minoru Kihara alisema kuwa Takaichi hataomba msamaha.
“Huo ndio msimamo wa serikali na ifahamike kuwa masuala yanayohusu Taiwan yatasuluhishwa kupitia mazungumzo wala si kushambuliwa na China,” akasema Minoru
China imekuwa ikishinikiza itumie nguvu zake za kijeshi kutwaa kisiwa cha Taiwan ikidai ni eneo lake lakini serikali ya Taiwan nayo haitaki kuwa chini ya uongozi wa China.
Kutokana na uhasama huo unaoendelea, ubalozi wa Japan uliwaambia raia wake China waheshimu sheria ya nchi hiyo lakini wajihadhari katika kutangamana na wazawa.
Iliwataka raia wake wazingatie usalama wao wakiwa nje, wasisafiri pekee yao na wamakinikie usalama wa watoto wao.
China nayo inalenga kutikisa uchumi wa Japan baada ya kuwaomba raia wake wasisafirie hadi nchi hiyo.
Raia wa China huchangia idadi ya juu ya watalii wanaoenda Japan na ikiwa ni zaidi ya robo ya watalii wote.
Zaidi ya mashirika 10 ya ndege za China zimekatiza safari za watalii wanaoelekea Japan hadi Disemba 31 na abiria ambao walikuwa wamelipia tiketi za ndege wamerejeshewa hela zao.