Kimataifa

Heche, vinara wengine Chadema waachiliwa huru nchini Tanzania

Na REUTERS November 12th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

DAR ES SALAAM, TANZANIA

POLISI nchini Tanzania mnamo Jumanne waliwaachilia wanasiasa wanne wakuu wa upinzani ambao walikamatwa wakidaiwa kuchochea maandamano nchini humo.

Maandamano hayo yalishuhudiwa wakati wa uchaguzi wa mwezi uliopita ambapo Rais Samia Suluhu alitangazwa mshindi wa urais kwa asilimia 98 ya kura.
Kati ya wale ambao waliachiliwa huru kwa dhamana ni Naibu Mwenyekiti wa CHADEMA, chama kikuu cha upinzani Tanzania, John Heche.
Kiongozi huyo alinyakwa mnamo Oktoba kwa tuhuma za kushiriki ugaidi kwa mujibu wa wakili wake.
Masaibu ya Heche pia yalishuhudiwa akizuiwa na maafisa wa usalama kuhudhuria mazishi ya aliyekuwa Waziri Mkuu wa Kenya marehemu Raila Odinga mwezi uliopita.
Alizuiliwa kwenye afisi za uhamiaji katika mpaka wa Kenya na Tanzania, Isebania, Kaunti ya Migori.
Amani Golugwa ambaye ni naibu katibu mkuu wa Chadema pia aliachiliwa huru baada ya kunyakwa wikendi kwa tuhuma hizo hizo za kushiriki ugaidi.
Chadema kupitia mtandao wake ilichapisha habari za kuachiliwa huru kwa Golugwa.
Kiongozi wa Chadema, Tundu Lissu, naye bado anapambana mahakamani baada ya kushtakiwa kwa ugaidi mnamo Aprili.
Kuzuiwa kushiriki uchaguzi wa mwezi uliopita ni kati ya sababu ambazo zinadaiwa zilichochea maandamano na kusababisha uchaguzi Tanzania uvurugike katika baadhi ya maeneo.
Mnamo Ijumaa, zaidi ya watu 145 walishtakiwa kwa uhaini baada ya kushiriki maandamano hayo.
Zaidi ya watu 170 nao walishtakiwa hapo awali kutokana na hasara na fujo ambazo zilitokea wakati wa maandamano.
Kwa mujibu wa Chadema na mashirika ya kijamii, zaidi ya watu 1,000 walipigwa risasi wakati wa maandamano hayo.
Hata hivyo, serikali haijakubali hilo na imekimya kabisa kuhusu takwimu za waliouawa.
Badala yake, serikali ilisema idadi hiyo ya watu 1,000 iliongezwa na kutiwa chumvi ila haionekani iwapo itatoa takwimu zake kuhusu waliouawa na maafisa wa usalama.
Mashirika kadhaa ambayo yalishuhudia uchaguzi huo yalitilia shaka uwazi wake huku Samia naye akipambana kuhalalisha ushindi wake machoni mwa jamii ya kimataifa.
Waangalizi wa Umoja wa Afrika (AU) walitoa taarifa ambapo walisema uchaguzi huo haukuwa na uwazi wowote. AU ilisema waangalizi wake walizuiwa kuingia katika baadhi ya vituo vya kuhesabu kura na kusema masanduku yalikuwa yakijazwa tu kura.
Muungano wa Mataifa ya Kusini mwa Afrika (SADCC) nao ulisema kuwa uchaguzi huo ulikuwa aibu na haukutimiza vigezo vya kidemokrasia.
Rais Samia aliapishwa Novemba 3 katika hafla ambayo ilisusiwa na marais wengi wa Afrika wakiwemo wale kutoka Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC). Ni marais wa Zambia, Burundi, Msumbiji na Somalia pekee ndio walihudhuria.