Serikali yaonya wanaohangaisha wakulima wa kahawa
Na MWANGI MUIRURI
VYOMBO vya usalama katika ukanda wa Mlima Kenya vimepanga kusambaratisha kabisa njama za wezi wa kahawa ambao huwasababishia wakulima hasara ya Sh3 bilioni kwa mwaka.
Kwa mujibu wa mshirikishi wa usalama eneo hilo, Wilson Njega ambaye alizungumza na Taifa Leo Dijitali ni kuwa serikali imekuwa ikifanya udadisi wa hali hiyo ya wizi wa kahawa na kugundua kuwa huwa ni njama kati ya wasimamizi wa viwanda vya kahawa na wakora wengine katika mtandao wa biashara ya kahawa.
“Katika hali hiyo, tumetoa onyo kwa wasimamizi wote wa viwanda kuwa ni laziwa wawe wakitufahamisha kuhusu kiwango cha kahawa ambayo iko katika mabohari yao na siku ambayo inanuiwa kuwasilishwa hadi sokoni,” akasema Bw Njega.
Alisema kuwa wale wasimamizi ambao hawatakuwa wakifanya hivyo, na kahawa hiyo iishie kuibiwa, “basi hao wasimamizi ndiyo katika mtazamo wetu watawajibishwa kuhusiana na wizi huo.”
Alisema kuwa baada ya kufahamishwa kuhusu kahawa katika stoo za viwanda hivyo, maafisa wa usalama watakuwa na uwezo wa kuweka mikakati ya kuilinda.
“Jinsi tutakavyozidi kuimarisha ulinzi huu, tutapendekeza kuwa kahawa yote ambayo iko katika usimamizi wa shirika moja la wakulima iwe ikihifadhiwa katika stoo moja. Sisi tutakuwa tukitoa ulinzi katika harakati za kuisafirisha hadi katika stoo hiyo na pia ikibidi, tuwe tunaisidikiza hadi sokoni,” akasema.
Kupangwa
Bw Njega alisema kuwa wizi wa kahawa hupangwa na wandani wa mashirika ya kahawa ya wakulima na ambapo mwanya mmoja ambao hutumika ni kukosa kufahamisha vyombo vya usalama kuhusu kuweko kwa kahawa katika stoo.
Mwaka wa 2011, aliyekuwa Katibu katika Wizara ya Usalama wa Ndani, Francis Kimemia ambaye kwa sasa ni Gavana wa Kaunti ya Nyandarua alitangaza harakati za kuundwa kwa kikosi maalum cha kupambana na wizi wa kahawa.
Aidha, alitangaza kuwa kulikuwa na nia ya kuundwa kwa sheria za kuwindana na wezi wa kahawa nchini na ambapo adhabu dhidi ya mwizi ilikuwa iwe miaka 10 gerezani au faini ya Sh5 milioni au zote mbili.
Kwa mumiliki wa leseni ya usagaji kahawa na ambaye angenaswa akiwa katika njama ya wizi wa kahawa ya wakulima, adhabu ingekuwa kupokonywa leseni au faini ya Sh10 Milioni au kifungo cha miaka 10 gerezani au hali zote tatu kwa mpigo mmoja.
Hata hivyo, tangazo hilo la Kimemia halikutimizwa na wizi wa kahawa umekuwa changamoto kuu ya kuafikia pato kwa mkulima wa kahawa ambaye kila mwaka amekuwa akilia kuhusu kupunguka kwa pato, hali ambayo huangazia sekta hii ya kilimo kuwa ya utumwa.