Serikali imekopa Sh3 trilioni chini ya utawala wa Ruto- CBK
RIPOTI ya Benki Kuu ya Kenya (CBK) iliyowasilishwa bungeni imeonyesha kuwa serikali ya Kenya Kwanza chini ya Rais William Ruto imekopa angalau Sh3 trilioni ndani ya kipindi cha miaka mitatu.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo iliyowasilishwa mbele ya Kamati ya Madeni ya Umma na Ubinafsishaji wa Mashirika ya Umma inayoongozwa na Mbunge wa Balambala, Abdi Shurie, deni la Kenya lilikuwa Sh8.7 trilioni katika mwaka wa fedha 2021/22—wakati Rais Ruto alipoingia madarakani.
Kufikia Juni 30, 2025 deni hilo lilikuwa limepanda hadi Sh11.81 trilioni, ongezeko la asilimia 17, huku serikali ikiegemea zaidi mikopo ya ndani ili kujaza mapengo ya bajeti.
CBK imebainisha kuwa matarajio ya ukopaji wa ndani yamekuwa “makubwa mno” katika kutimiza mahitaji ya kifedha ya serikali. Kwa wastani, serikali imekuwa ikikopa takribani Sh1 trilioni kila mwaka tangu 2022.
Ripoti hiyo hata hivyo haionyeshi miradi yoyote mahsusi iliyofadhiliwa kwa Sh3 trilioni zilizokopwa ndani ya miaka hii mitatu.
Kwa sasa, deni la taifa linajumuisha Sh6.33 trilioni (mikopo ya ndani) na Sh5.5 trilioni (mikopo ya kigeni).
Rais Ruto alipoapishwa mnamo Septemba 13, 2022, aliahidi mageuzi yakuleta nidhamu ya matumizi ili kudhibiti ukopaji, hasa wakati uchumi ulikuwa ukikabiliwa na changamoto za ukame, mafuriko na athari zilizotokana na Covid-19.
Deni la Kenya lilikuwa Sh7.7 trilioni katika mwaka wa fedha 2020/21, na likapanda kwa Sh1.1 trilioni 2021/22 kabla ya kuongezeka zaidi chini ya utawala wa Kenya Kwanza.
Kwa sasa, uwiano wa deni kwa pato la taifa (GDP) umefikia asilimia 69, kiwango kinachozua wasiwasi mkubwa.
Mwezi Oktoba 2023, Bunge liliondoa kiwango ch juu cha deni cha Sh10 trilioni na kuiweka kuwa asilimia 55 kwa Pato ya Taifa hatua iliyolenga kuboresha nidhamu ya matumizi lakini isiruhusu serikali kuendelea kukopa.
Riba inayolipwa kwa mikopo ya ndani imepanda kwa kasi, ishara ya serikali kutegemea pakubwa ukopaji wa ndani—ambao kwa kiasi kikubwa unanyima biashara ndogo nafasi ya kupata mikopo nafuu.
Malipo ya riba ya mikopo ya ndani yalikuwa:Sh388.8 bilioni (2020/21), Sh456.8 bilioni (2021/22), Sh533.1 bilioni (2022/23), Sh622.5 bilioni (2023/24 na Sh776.3 bilioni (2024/25).
Malipo ya riba ya mikopo ya ndani yameongezeka kwa asilimia 24.7 mwaka 2024/25 pekee, hasa kutokana na mzigo wa riba kwenye hati za dhamana za serikali.
Kwa sasa, sehemu kubwa ya mapato ya serikali inaelekezwa kulipa madeni badala ya huduma muhimu kwa wananchi,jambo linaloongeza hofu kuhusu mwelekeo wa uchumi. Gavana wa CBK, Dkt Kamau Thugge, amesisitiza kuwa japokuwa deni linabaki kuwa katika kiwango kinachofaa bado nchi iko kwenye “hatari kubwa ya kusongwa na madeni,” hasa kutokana na mapato ya serikali kukosa kufikia malengo.
Hata hivyo, amedokeza kuwa serikali itaendeleza mageuzi katika soko la ndani la madeni ili kupunguza misukosuko, ikiwa ni pamoja na kupanuwa wigo wa wawekezaji katika hati za dhamana, kubuni bidhaa mpya za uwekezaji zinazolenga makundi tofauti, kuboresha upatikanaji na ufanisi wa masoko ya dhamana za serikali
Huku mikopo ikiongezeka na uchumi ukiendelea kukabwa na mzigo wa ulipaji riba, wadadisi wanahoji iwapo serikali itafanikiwa kusawazisha ukuaji wa uchumi na kudhibiti deni bila kutishia ustawi wa wananchi na sekta ya biashara.