• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 10:08 PM
NJAA: Kiangazi kikali kinavyoendelea kutatiza maelfu ya wananchi

NJAA: Kiangazi kikali kinavyoendelea kutatiza maelfu ya wananchi

Na BERNARDINE MUTANU

MAELFU ya wananchi wanakabiliwa na njaa kutokana na upungufu wa mvua ya vuli kulingana na ripoti mpya ya Mamlaka ya Kudhibiti hali ya Ukame Nchini (NDMA).

Hii ni kinyume cha ilivyokuwa imetabiri idara ya kutabiri hali ya hewa ambayo katika ripoti ilisema kuwa maeneo mengi nchini yangepata mvua nyingi.

Takriban kaunti 23 zinakabiliwa na ukame, wiki chache tu baada ya mvua ya vuli kukoma.

Kaunti zilizoko kwenye maeneo kavu ndizo zimeathiriwa zaidi na wakazi wa maeneo hayo wanafaa kutarajia kupungua kwa chakula, maji na malisho ya mifugo katika majuma kadhaa yajayo.

NDMA ilitoa tahadhari kwa kaunti saba huku ripoti hiyo ikionyesha kuwa kiwango cha chakula kimekuwa kikipungua kutoka Novemba wakati ambapo ni kaunti tatu pekee zilizokuwa zimepewa tahadhari kuhusiana na hali ya ukame na ukosefu wa chakula.

Kaunti ambazo hali ya ukame inazidi ni Kitui, ingawa hali inaimarika kwa sababu ya mvua fupi, Turkana, Marsabit, Samburu na Tana River.

Hali ya ukame inazidi kuwa mbaya zaidi kaunti kaunti za Garissa na Tharaka, ilionya NDMA.

Ingawa hali ya ukame katika kaunti zingine 16 ambazo ni kame imeorodheshwa kuwa ya kawaida, ni Kaunti ya Kwale pekee ambayo hali yake inaimarika.

Kati ya kaunti ambazo ziliorodheshwa miongoni mwa zilizo na hali ya kawaida ya ukame, Mandera, Wajir, West Pokot, Meru (Kaskazini) na Kilifi hali inazidi kuwa mbaya zaidi ilhali hali ni dhabiti Isiolo, Laikipia, Taita Taveta, Lamu, Embu (Mbeere), Kajiado, Baringo, Makueni, Nyeri (Kieni) na Narok.

“Upungufu wa chakula unatokana na mvua chache iliyonyesha mwezi wa Desemba,” ilisema MDMA katika ripoti hiyo.

Idara ya kutabiri hali ya hewa katika ripoti mwaka jana ilitabiri kuwa, “Maeneo mengi nchini yatapata mvua nyingi na nzuri. Hii itakuwa hasa Kaskazini Mashariki, Kaskazini Magharibi, Magharibi, Kati na Pwani.”

Hata hivyo kulingana na NDMA, “Mvua fupi kati ya Oktoba na Desemba ilianza ikiwa imechelewa, ilikuwa mbaya na haikunyesha maeneo mengi kama ilivyotarajiwa na kulikuwa na ukame ulioathiri mimea katika kaunti kame.”

Katika kaunti kama Kitui, Baringo, Laikipia na Nyeri (Kieni) kuchelewa kwa mvua, na ukame uliofuatia ulisababisha mimea kumea vibaya hali iliyolazimisha wakulima kupanda tena.

Asilimia 80 ya wakulima Kieni, “Hata hivyo hawakupanda tena kwa sababu ya gharama kubwa ya nyenzo za kilimo, hali iliyosababisha kiwango cha mazao eneo hilo kudidimia zaidi.”

Wafugaji wanaathirika zaidi kwani inawabidi kwenda masafa marefu kutafuta maji kwa sababu mabwawa hayakuingia maji ya kutosha msimu uliokamilika.

Kaunti zilizoathirika zaidi ni Turkana, Garissa, Tana River, Samburu, Kajiado, Kilifi, Baringo, Kwale, Narok, Makueni and Meru (Meru Kaskazini).

Mwanamke abeba maji baada ya kutembea mchana kutwa kutoka Mto Kerio uliopo Elegeyo Marakwet hadi Chesotim, Tiaty, Kaunti ya Baringo Februari 16, 2019. Picha /Cheboite Kigen

“Upungufu wa mvua wakati wa mvua ya vuli umeathiri vibaya hali ya maji na malisho. Pia imepunguza chakula na maziwa, hali inayotarajiwa kuathiri uwepo wa chakula mpaka mvua ya masika inayotarajiwa kuanza Machi 2019,” ilisema NDMA.

Kwa sababu ya mvua nyingi iliyoshuhudiwa katika ya Machi na Mei 2018, chakula kiliimarika nchini.

Hata hivyo, “Chakula kinapungua kwa sababu ya upungufu wa mvua kati ya Oktoba na Desemba,” ilisema ripoti hiyo.

Ingawa hali chakula imeimarika nchini kwa jumla, bado hatua madhubuti zaidi zinafaa kuchukuliwa kulingana na ripoti kuhusu hali ya chakula ulimwenguni.

Kati ripoti hiyo, Kenya iliorodheshwa nambari 77 katika orodha ya mataifa 119 yanayoendelea.

Kulingana na ripoti hiyo, hali ya chakula nchini Kenya sio nzuri sana na bado ni ya kutisha ambapo Mkenya mmoja kati ya watatu (14.5 milioni) huathirika kutokana na ukosefu wa muda mrefu wa chakula na virutubishi vinavyohitajila kila mwaka.

Umaskini

Ripoti hiyo inasema kuwa hali ya kukosekana kwa chakula cha kutosha imesababishwa na usimamizi mbaya, mabadiliko ya hali ya hewa na umaskini mkubwa.

Ripoti hiyo ilitolewa huku utafiti ukionyesha kuwa joto linazidi ulimwenguni, hali inayoweza kuathiri uwepo wa chakula.

“Ingawa hali imeimarika kwa jumla, bado njaa na ukosefu wa virutubishi inatia hofu hasa kutokana na umaskini, mabadiliko ya anga na majanga mengine,” ilisema ripoti hiyo.

Sio tu mabadiliko ya hali ya hewa yamesababisha mazao kutofanya vyema, yameathiri pia samaki baharini na wavuvi ambao hutegemea samaki hao kwa chakula na chumo.

“Njaa imekuwa nyingi katika mataifa ambayo hutegemea mvua na hali nzuri ya hewa katika kilimo,” lilisema Shirika la Chakula Ulimwenguni (FAO) katika ripoti yake kuhusu usalama wa chakula na virutubisho iliyotolewa Septemba 2018.

Kulingana na FAO, watu ambao wameathirika kutokana na ukosefu wa chakula ulimwenguni ni milioni 821 na barani Afrika, ukosefu wa chakula unaendelea kuongezeka katika maeneo yote.

You can share this post!

UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Sifa bainifu zinazodhihirisha...

AKILIMALI: Mazeras stones yalivyoteka soko la ufundi

adminleo