Makala

Mauaji mjini Nakuru yazua hofu genge la Confirm limefufuka

Na MERCY KOSKEI December 6th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

HUKU Nakuru ikijiandaa kwa shamrashamra za Krismasi, wimbi jipya la mauaji na mashambulizi limeanza kutikisa mitaa yake na kufufua hofu ya kurejea kwa genge hatari la Confirm lililowahi kuhangaisha kaunti hiyo.

Desemba 1, 2025, watu wawili waliuawa katika visa viwili tofauti vinavyoshukiwa kuwa mashambulizi ya kulipiza kisasi na mabaki ya genge hilo katika maeneo ya Kwa Rhonda na Flamingo, katika mauaji yaliyotekelezwa kwa ustadi wa magenge.

Rodgers Marucha, 25, alidungwa visu mara kadhaa na washambuliaji waliomfahamu kabla ya mwili wake kutupwa eneo la Sewage, Kwa Rhonda. Wahalifu hao—wanaodaiwa kuwa marafiki zake wa zamani—walipigia familia simu na kuwaambia “waende wachukue mzigo wao.”

Kilomita chache kutoka hapo, kundi lingine lilivamia nyumba ya kijana Henry Ongae, 18, katika mtaa wa Flamingo na kujaribu kumteka, lakini alipiga kengele. Walimdunga shingoni mara kadhaa. Alikimbizwa katika Hospitali ya Rufaa ya Nakuru, ambako alithibitishwa kufariki.

Vifo vyao vimeongeza taharuki katika mitaa ambayo tayari ilikuwa inatatizwa na wimbi la wizi wa usiku, mashambulizi ya visu na makabiliano ya magenge yanayolipiziana kisasi.

Kwa wenyeji wengi, matukio haya yanawakumbusha makali ya enzi za genge la Confirm lililotawala mitaa ya kipato cha chini kati ya 2018 na 2022, likihusika na wizi wa simu, utapeli, mihadarati, ukatili na unyakuzi.

Genge hilo lilivutia vijana wadogo, wengine wakiwa na umri wa miaka 13. Kati ya makabiliano ya maeneo na ibada za siri, polisi waliwahi kulihusisha na mauaji, ubakaji, utekaji, uporaji na mfululizo wa watu kupotea katika maeneo kama Kivumbini, Lake View, Rhonda, Flamingo na Kaptembwa.

Baada ya malalamishi mengi kutoka kwa wananchi, aliyekuwa Naibu Kamanda wa Polisi Kasarani, Peter Mwanzo, alipandishwa cheo na kupelekwa Nakuru mnamo Juni 29, 2022, na aliyekuwa Waziri wa Usalama wa Ndani Dkt Fred Matiang’i kurejesha utulivu.

Leo hii, hali bado ni ya wasiwasi maeneo ya Kwa Rhonda, maduka yakifungwa mapema na waendeshaji boda boda wakiepuka njia fulani baada ya jioni.

Licha ya polisi kusema uchunguzi umeanzishwa, wakazi wanasema wahalifu hao hawakuwa “wezi wa kawaida.” Ustadi na haraka yao, wanasema, unafanana kabisa na mbinu za Confirm.

“Tumeanza kuona sura mpya, vijana wakijikusanya kwenye makundi, wengine wakiwa na visu. Mashambulizi yanaonekana kupangwa—sio ya bahati mbaya. Hivi ndivyo Confirm ilianza,” alisema mkazi mmoja wa Kwa Rhonda.

Mitaa mingi ya kipato cha chini Nakuru ina idadi kubwa ya vijana wasio na ajira, hali inayowafanya kuwa rahisi kushawishiwa kujiunga na magenge, hasa msimu wa sikukuu unapoanza na uhalifu kuongezeka.

Pombe kali za bei rahisi na dawa za kulevya zinapatikana kwa urahisi, na vijana wengi hushawishika kujiunga na vikundi vinavyoahidi ulinzi, umaarufu na pesa za haraka.

Mkazi mwingine, aliyekataa kutajwa, alisema mpango wa Nyumba Kumi umevurugika kutokana na hofu ya kulengwa na magenge.

“Tunachotaka ni amani. Watu wanaogopa kuongea, ukitoa taarifa unalengwa na unaweza kulipiziwa kisasi,” alisema.

Kihistoria, uhalifu Nakuru huongezeka kila mwezi wa Desemba kutokana shughuli za usiku na wageni wanaokuwa rahisi kushambuliwa.

Hata hivyo, polisi wanaonya kuwa ni mapema kuhusisha mauaji haya na kurejea kwa Confirm.

Kamanda wa Polisi Kaunti ya Nakuru, Emmanuel Opuru, alisema wanafanya uchunguzi kujua uhusiano uliopo kati ya visa hivyo viwili.

“Tunazichukulia kama kesi mbili tofauti kwa sasa,” alisema.

Ripoti ya 2025 ya Shirika la Kitaifa la Takwimu la Kenya (KNBS) imeiweka Nakuru katika nafasi ya nne nyuma ya Nairo