Akili Mali

Anaunda bidhaa za thamani kwa kutumia sehemu za nazi

Na PETER CHANGTOEK December 9th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

WENGI hawajui thamani ya vifuu vya nazi.

Vifuu hivyo, mara nyingi huchukuliwa na wengi kama taka zinazochafua mazingira.

Hata hivyo, MacDonald Ngala, 36, kutoka eneo la Mariakani, Kilifi, huvitumia vifuu hivyo pamoja na sehemu nyinginezo za nazi kuzitengeneza bidhaa zenye thamani.

Huzitengeneza bidhaa kama vile maua ya kurembesha maskani, mbali na bidhaa nyinginezo kutokana na vifuu hivyo, na kuwauzia wateja kutoka maeneo mbalimbali katika eneo la Pwani ya Kenya.

Hutengeneza kobe, maua, samaki, glasi za kunywea mvinyo, vikombe, majagi, vifaa vya kuweka sabuni, na kadhalika.

 

MacDonald akionyesha bidhaa anazozitengeneza katika eneo la Mariakani. PICHA/PETER CHANGTOEK

Anadokeza kuwa, amekuwa akizitengeneza bidhaa hizo kwa muda wa miaka minne. “Siku moja nilipata vifuu vya nazi vikiwa vimetupwa na vimeliwa na mchwa. Nikachukua; nikaangalia, nikaona vimeliwa na mchwa hadi vimebakishwa, nikaona hicho ni kitu kigumu sana,” asema MacDonald.

Anaongeza kuwa, baada ya kuvitazama vifuu hivyo kwa muda, akawa na shauku moyoni ya kutengeneza bidhaa kutokana navyo.

“Nimegundua kuwa, kumbe huu mti wa mnazi una thamani kubwa,” asema, akiongeza kuwa, alianza kuvitengeneza viti vya ajabu kutokana sehemu fulani ya minazi, kisha akaanza kuvitumia vifuu kuvitengeneza vipuli.

Alipoanza kuzitengeneza bidhaa zake, watu walikuwa wakienda kuziangalia tu, na hawakuwa wakizinunua, ikabidi ahamishe shughuli hiyo hadi eneo jingine lililoko mjini Mariakani.

“Kuna shirika fulani ambalo lilikuwa limenichukua katika maonyesho katika Uga wa Mkomani. Liliona kuwa ninaongeza thamani kwa mti wa mnazi. Nikaona kuwa kumbe kifuu kinatengeneza makaa na kuna mafuta ambayo yanatengenezwa kutoka kwa nazi. Nilikuwa nikitumia nazi vibaya kwa sababu nilikuwa nikinunua nazi halafu ninakata na kuwagawia watu,” asema.

Anaongeza kwamba kuna mashine ambayo anahitajika kuwa nayo ili kuanza kuzitumia nazi kuyatengeneza mafuta.

“Nazi moja inaweza kutengeneza pesa nyingi sana,” asema MacDonald, akiongeza kuwa, hupata malighafi kutoka sehemu tofauti tofauti, kama vile katika hoteli na kutoka kwa watu binafsi, ambapo hununua kwa bei nafuu.

Baadhi ya bidhaa zinazotengenezwa na MacDonald. PICHA/PETER CHANGTOEK

Anafichua kuwa alikisoma kitabu kilichoandikwa na Irene Mureithi kinachoitwa Celebrate the Hard Times kilichomtia moyo, ndiposa akaamua kukitumia kipaji chake vyema kuzitengeneza bidhaa aina ainati kutokana na sehemu tofauti tofauti za mnazi.

“Niligundua kuwa, ukitambua kipawa chako, mambo huwa rahisi kuliko kukaa. Nikawa ninafunza shule fulani wanafunzi jinsi ya kugundua talanta zao. Nikasoma kitabu kingine cha Robert Asewe kutoka Uganda,” asema, akiongeza kuwa baada ya kuvisoma vitabu hivyo, akawa na motisha zaidi.

Huuza bidhaa zake kwa bei tofauti tofauti. “Huuza yale maua meupe kwa Sh2,000, kila moja, la njano ni Sh1,800, na kuna yale ya Sh1,500. Huuza jozi moja ya vipuli kwa Sh200,” afichua MacDonald, ambaye pia huuza mkufu mmoja kwa Sh350, na bangili kwa Sh250 kila moja.