Serikali ilivyochezea wauguzi
Na BENSON MATHEKA
MGOMO wa wauguzi ulianza kufifia Alhamisi baada ya kuibuka kuwa walidanganywa kwenye mkataba wa pamoja waliotia sahihi na Serikali na Baraza la Magavana (CoG) mnamo 2017.
Hii ni baada ya Serikali kusema kuwa hata kaunti nne ambazo zimetekeleza mkataba huo zimefanya hivyo kinyume cha sheria, na hivyo zinapasa kusimamisha malipo hayo mara moja, na kurudisha fedha zote ambazo tayari zimewalipa wauguzi wao.
Matukio haya yanaonyesha kuwa Serikali na CoG walitumia hila na udanganyifu dhidi ya wauguzi.
Alhamisi, wauguzi katika kaunti za Bomet na Kakamega walirejea kazini baada ya serikali kusisitiza kwamba haina pesa za kuwalipa marupurupu waliyodai.
Cha kutamausha zaidi ni agizo la Mwelekezi wa Bajeti, Agnes Odhiambo ambaye amesema hatua ya kaunti nne kutekeleza mkataba wa 2017 ni kinyume cha sheria, kwa sababu marupurupu hayo hayakuidhinishwa na Tume ya Mishahara ya Watumishi wa Umma (SRC).
Hii inaonyesha kuwa Serikali ilifahamu kuwa mkataba huo ulikuwa feki kwa vile ilipoweka sahihi ilifaa kwanza kupata ushauri wa SRC.
Kwenye barua aliyoandikia kaunti za Migori, Machakos, Mombasa na Kwale, Bi Odhiambo anasema wauguzi hawafai kulipwa marupurupu ambayo hayajaidhinishwa na SRC.
“Ofisi yangu ina habari kwamba baadhi ya kaunti zinalipa wauguzi marupurupu kinyume cha yale yaliyoidhinishwa na SRC. Kulipa marupurupu bila idhini ya SRC ni kinyume cha sheria,” alionya Bi Odhiambo.
Mwenyekiti wa SRC, Lyn Mengich kwa upande wake anasema serikali za kaunti zinahitaji Sh3.5 bilioni kila mwaka kuwalipa wauguzi marupurupu wanayodai lakini pesa hizo hazipo.
Walipotangaza mgomo na kutaka CoG kusaidia kuhakikisha serikali za kaunti zimeheshimu mkataba huo, baraza hilo liliwakana wauguzi likisema wameajiriwa na kaunti husika na hivyo haliwezi kuingilia.
‘Hakuna pesa’
Rais Uhuru Kenyatta na mwenyekiti wa sasa wa COG Wycliffe Oparanya pia wanasisitiza kuwa serikali haina pesa za kulipa marupurupu hayo.
Hata hivyo Bw Panyako anapuuza kauli yao na ya Bi Odhiambo akisema hafai kuelekeza serikali za kaunti zinavyopaswa kuhudumu.
Ni chama chake pekee kinachorejelea mkataba wa 2017 ambao anasisitiza ni lazima utekelezwe kabla ya wauguzi kurejea kazini. Serikali na CoG hazionekani kuutambua.
“Kwa nini kila mtu anataka kuzungumzia mgomo wa wauguzi. Tulitia sahihi mkataba na serikali za kaunti na unafaa kutimizwa. Hatutaki kujua utatimizwa lini lakini ni lazima utimizwe. Tutapiganie haki za wauguzi wetu,” alisema.
Bw Panyako na maafisa wengine wa chama hicho, wameitwa kufika mbele ya mahakama kueleza kwa nini wasiadhibiwe kwa kukaidi agizo la kusitisha mgomo huo.