POLISI wametoa maelezo mapya kuhusu kifo cha mwanasiasa na mfanyabiashara Cyrus Jirongo, wakieleza matukio yaliyosababisha ajali ya barabarani iliyomuua wakisema dereva wa basi lililogongana na gari lake huenda atashtakiwa.

Kupitia taarifa, Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI), ilisema Jirongo alifariki baada ya kujeruhiwa vibaya katika ajali ya barabarani iliyotokea usiku wa Desemba 13, 2025, katika eneo la Karai kando ya barabara kuu ya Nakuru–Nairobi.

Ajali hiyo ilihusisha gari lake binafsi, lenye nambari ya usajili KCZ 305U, na basi la uchukuzi wa umma (PSV) la kampuni ya Climax Company Ltd, lenye nambari KCU 576A.

Dereva wa basi hilo, Tyrus Kamau Githinji, sasa anachunguzwa kwa kosa la kusababisha kifo kwa kuendesha gari bila uangalifu, DCI ilisema.

Kwa mujibu wa uchunguzi wa awali uliojumuisha uchambuzi wa kanda za kamera za CCTV, ajali hiyo ilitokea takribani saa nane na dakika kumi na tisa usiku 2:19, gari la Bw Jirongo lilisukumwa umbali wa takribani mita 25 kutoka mahali pa ajali.

Basi lilisimama takribani mita 50 kutoka eneo la ajali. Bw Jirongo alikuwa peke yake kwenye gari wakati wa ajali hiyo.

DCI ilisema kikosi cha pamoja cha wapelelezi wa mauaji na wataalamu wa uchunguzi wa kisayansi kutoka Maabara ya Kitaifa ya Uchunguzi wa Uhalifu kilitumwa eneo la tukio muda mfupi baada ya ajali.

Timu hiyo ilifanya uchunguzi wa mapema na kukusanya vielelezo muhimu kwa upelelezi.

Wapelelezi pia walipata na kuchambua kanda za CCTV kutoka Kituo cha Mafuta cha Eagol, ambazo zimekuwa muhimu katika kubaini hatua za mwisho za marehemu Jirongo.

Kanda za CCTV zilionyesha kuwa Bw Jirongo aliingia kituo hicho cha mafuta akitokea upande wa Nairobi saa nane na dakika kumi na nane usiku, lakini hakuweka mafuta.

Saa nane na dakika kumi na tisa alisimama kwa muda mfupi katika lango la kutoka kabla ya kugeuka kulia sekunde chache baadaye kuelekea Nairobi.

Sekunde sita baadaye, kamera zilinasa basi likigonga gari lake.

Tangu wakati huo, wapelelezi wamemhoji Bw Githinji, ambaye awali aliandikisha taarifa kwa trafiki katika kituo cha polisi cha Naivasha na kuachiliwa kwa dhamana ya pesa taslimu huku uchunguzi ukiendelea.

Ameagizwa kuripoti tena katika kituo hicho mnamo Desemba 22, 2025, kwa hatua zaidi za polisi.

Wapelelezi pia wamemhoji mlinzi wa usiku wa kituo cha mafuta na mhudumu, ambao wote walitoa simulizi zao binafsi kuhusu matukio ya usiku huo.

Katika taarifa nyingine, DCI ilisema uchunguzi bado unaendelea, huku timu ya wataalamu ikitarajiwa kurejea eneo la ajali kwa uchambuzi zaidi.

Wapelelezi pia wanachunguza mienendo ya Bw Jirongo kabla ya ajali, ikiwemo kuandikisha taarifa kutoka kwa watu aliokutana nao mapema usiku huo.
Miongoni mwa maeneo yanayochunguzwa ni mkutano aliohudhuria katika Karen Oasis Bar and Restaurant jijini Nairobi, ambapo wapelelezi wanajaribu kubaini ratiba kamili ya mienendo yake.

Taarifa zaidi pia zinachukuliwa kutoka kwa abiria waliokuwa ndani ya basi la kampuni ya Climax na mashahidi wengine.

Baada ya uchunguzi kukamilika, faili kamili ya polisi itaandaliwa na kuwasilishwa kwa Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) kwa ushauri, DCI ilisema.

Mazingira ya kifo cha BW Jirongo yamezua wasiwasi miongoni mwa umma, hasa baada ya watu wa familia na marafiki wa karibu kuuliza maswali kuhusu jinsi alivyoishia Naivasha, ilhali aliripotiwa kuwa aliondoka Karen usiku akielekea nyumbani Gigiri.

Familia imekaribisha kuhusishwa kwa wataalamu na kutolewa kwa matokeo ya awali, lakini imesisitiza kuwa maswali yote ambayo hayajajibiwa lazima yashughulikiwe.

Katika taarifa yake, DCI ilituma rambirambi kwa familia, marafiki na jamaa wa Jirongo, na kuhakikishia umma kuwa imejitolea kufanya “uchunguzi wa kina, usio na upendeleo na unaoaminika” kwa mujibu wa Katiba ya Kenya na utawala wa sheria.