FAMILIA ya aliyekuwa Mbunge wa Likuyani, Dkt Enock Kibunguchy inataka uchunguzi wa ndani ufanywe kuhusu kifo chake cha ghafla, kauli ambayo inaibua madai kuwa huenda mauti yake yaligubikwa na utata.

Kwa mujibu wa ripoti kutoka Hospitali ya Eldoret, mbunge huyo alifariki kutokana na sumu kwenye chakula chake. Sumu hiyo ilimsababishia maradhi na akalazwa hospitalini.

Hata hivyo, familia yake imekataa ufafanuzi huo na unataka kujua matukio yaliyozingira kuugua kwake.

Dkt Kibunguchy aliaga dunia Hospitali ya Eldoret baada ya kuwa kwenye chumba cha wagonjwa mahututi kwa siku 10.

Nduguye mdogo Johnstone Walubengo Kibunguchy aliongoza familia yake kusema madai yanayozingira kuugua na kufa kwake yanashangaza na yanazua maswali mengi.

Kufahamu ukweli, familia hiyo imetangaza kuwa inalenga kushirikisha wataalamu wa kibinafsi wa uchunguzi. Hasa wanataka kufahamu matukio yaliyosababisha kulazwa kwa mbunge huyo wa zamani na hatimaye kufariki kwake.

Dkt Kibunguchy alikuwa mwanasiasa mzoefu na mbunge ambaye mchango wake ulifahamika kutokana jinsi alivyowasilisha bungeni kuhusu masuala ya Lugari.

Mwanasiasa huyo alimbwaga Cyrus Jirongo katika uchaguzi wa 2002 kupitia Narc na akahudumu hadi 2007.

Bw Jirongo alimshinda katika uchaguzi wa 2007 na kurejea bungeni kupitia tikiti ya KADDU.

Wakati eneobunge hilo lilipogawanywa 2013, Bw Kibunguchy aliwania na kushinda ubunge wa Likuyani kupitia ODM.

Kwenye uchaguzi wa 2017 alitetea kiti chake na kushinda kupitia Ford Kenya hadi akahudumu mpaka 2022.

Katika chaguzi huo alibwagwa na Innocent Mugabe wa ODM.