Jinsi ya kulinda nyumba, mali yako dhidi ya wahalifu msimu huu wa sikukuu
HUKU baadhi ya Wakenya wakiwa mashambani (ushago) kwa sherehekea za Krismasi na Mwaka Mpya na familia zao, suala la usalama wa nyumba na mali walizoacha jijini linazidi kuwa muhimu.
Takwimu zinaonyesha kuwa Desemba ni msimu ambao visa vya uhalifu na wezi kuvunja nyumba hasa zile ambazo zimefungwa kwa muda huongezeka.
Akizungumza na Taifa Dijitali, Mkurugenzi wa Robisearch, kampuni ya kiteknolojia, Robert Manyala, anasema wizi hutokea kwa sababu wamiliki wa nyumba huacha dalili zinazoonyesha kuwa hawapo.
“Wezi huangalia ishara kama vile, lango lililofungwa kwa muda, taa zinazowaka mchana na usiku pamoja na ukimya wa ghafla. Hii inawaonyesha wezi kuwa watu hawapo,” anafafanua.
Manyala anaongeza kuwa licha ya watu wengi kufunga kamera za CCTV au mifumo ya kisasa ya usalama, changamoto kubwa ni kutotumia kikamilifu teknolojia hiyo.
“Wengine husafiri bila kuweka mikakati ya kuhakikisha kuwa nyumba yao iko salama hali inayofanya tukio la uhalifu kutambuliwa kuchelewa,” anasema.
Aidha, anaonya kuwa usalama bora ni ule unaochanganya teknolojia, watu na ushirikiano wa kijamii.
Kwa wanaosafiri na wale ambao tayari wamesafiri msimu huu, Manyala anapendekeza matumizi ya kamera za CCTV zenye ubora wa juu, mifumo ya kufungua na kufunga milango kwa mbali.
“Teknolojia hizi humwezesha mwenye nyumba kufuatilia mali yake kwa wakati halisi kupitia simu, popote alipo,” anasema.
Kwa mujibu wake, kamera za kisasa zinapaswa kuwa na uwezo wa kuonyesha matukio ya usiku, kutuma arafa za haraka, hifadhi salama ya kumbukumbu na kuunganishwa na mifumo mingine kama taa na kengele.
“Leo, CCTV si kwa kurekodi tu, bali ni kuzuia uhalifu na kukupa amani ya moyo,” anaeleza.

Hata hivyo, hofu ya udukuzi bado ipo miongoni mwa Wakenya.
Manyala anahakikisha kuwa mifumo ya Robisearch inalindwa kwa usimbaji wa taarifa, uthibitishaji wa hatua mbili na masasisho ya mara kwa mara ili kuzuia uingiliaji usioidhinishwa.
Kwa nyumba za mashambani ambako mtandao si wa kuaminika, anashauri matumizi ya kamera zenye hifadhi ya ndani, kengele za betri na mifumo ya arifa za SMS. “Hata bila intaneti, usalama unaweza kudumishwa,” anasema.
Anasisitiza pia umuhimu wa ulinzi wa jamii.
“Teknolojia inapounganishwa na uangalizi wa majirani kupitia vikundi vya WhatsApp au SMS, uhalifu hupungua kwa kiwango kikubwa.”
Kuhusu ajali za moto zinazohusishwa na umeme wa KPLC, Manyala anapendekeza matumizi ya soketi za kisasa na teknolojia inayoweza kutoa tahadhari ikiwa kuna moto au moshi au hata na zile zilizo na uwezo wa kuzima umeme kiotomatiki.
Kwa familia zenye bajeti ndogo, anasema suluhisho rahisi kama kamera za bei nafuu, kengele za betri na ushirikiano wa majirani vinaweza kuleta tofauti kubwa.
“Usalama hauhitaji kuwa ghali. Kinachohitajika ni mipango mizuri, matumizi sahihi ya teknolojia na ushirikiano wa kijamii,” anahitimisha Manyala, huku akiwatakia Wakenya heri za Mwaka Mpya 2026.