Habari Mseto

Juhudi za JKIA kusimamia uwanja zakwama

February 23rd, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na BERNARDINE MUTANU

WABUNGE wamekataa pendekezo la Shirika la Ndege la Kenya Airways (KQ) kutwaa uwanja wa Ndege wa JKIA kwa kuungana na Mamlaka ya Viwanja vya Ndege (KAA).

Kamati ya Uwekezaji wa Umma (PIC) ilisema hatua ya kuungana kwa KQ na KAA kutasababisha mamlaka hiyo kufilisika.

Lengo la kuunganisha KAA na KQ lilikuwa ni kulisaidia shirika hilo ambalo kwa muda limekuwa likipata hasara kuimarika kifedha.

“Kamati hii imeamua kuwa hakuna kubadilishana fedha kuhusiana na suala hili mpaka Bunge imalize uchunguzi wake. Tunamwomba Mhasibu Mkuu kuchunguza suala hilo haraka iwezekanavyo,” alisema mwenyekiti wa PIC na Mbunge wa Mvita Bw Abdulswamad Nassir.

Mwenyekiti wa KAA Johny Andersen aliwasilisha stakabadhi bungeni zilizoonyesha kuwa wakurugenzi wa KAA walihofia kuhusiana na pendekezo la KQ (PIIP), lililoonekana kuungwa mkono na Baraza la Mawaziri.

KAA, kila mwaka hukusanya Sh7 bilioni kutoka JKIA lakini ikiwa itaungana na KQ itakusanya Sh2.9 bilioni.

KQ inalenga kutwaa usimamizi wa uwanja wa ndege wa JKIA kwa muda wa miaka 30. Kwa muda wa miaka kadhaa iliyopita, KQ imekuwa ikipata hasara na pia imekuwa ikishuhudia marekebisho.