Magavana walia njaa Ruto akiwacheleweshea mgao wa kaunti
MAGAVANA wameonya kwamba kaunti ziko pabaya na zinakodolewa macho na usitishaji wa huduma, Serikali Kuu ikiwa bado haijatuma Sh68 bilioni kwa magatuzi hayo.
Kaunti huenda zikalemewa kulipa wafanyakazi mishahara yao, kuwasilisha makato ya wafanyakazi na kulemewa kulipa wanakandarasi na wawasilishaji bidhaa.
Hali hiyo inatokea wakati ambapo Muungano wa Wafanyakazi wa Kaunti Nchini (KCGWU) umetishia kuandaa mgomo.
Serikali za kaunti hazijapokezwa mgao wa Sh33.2 bilioni za Desemba 2025 na Sh35.27 bilioni za Januari 2026.
Mara ya mwisho kaunti kupokea pesa kutoka kwa serikali kuu ilikuwa Novemba 2025.
Gavana wa Nyeri Mutahi Kahiga alisema kuwa utawala wake umekuwa ukipambana kutoa huduma muhimu kwa sababu ya pesa kuchelewa.
Alitoa mfano wa kuanti kukosa hata pesa za mafuta ya magari yake mnamo Desemba na sasa hawawezi kuwalipa wawasilishaji bidhaa.
“Kwa sasa maafisa wa Kliniki wametoa notisi ya kushiriki mgomo pamoja na KCGWU. Kuchelewa kupokea hela hizo kutaharibu hali,” akasema Bw Kahiga.
“Tukicheleweshewa pesa, wale ambao wataathirika ni wananchi kwa kuwa hatutakuwa na pesa za kununua dawa hospitalini na mambo mengine muhimu,” akaongeza.
Gavana wa Makueni Mutula Kilonzo, naye alisema hali ni mbaya kiasi kwamba wamelazimika kukopa kwenye benki kufadhili shughuli za kaunti.
Aliongeza kuwa wataangushiwa riba ya juu iwapo watakosa kulipa hela hizo kwa wakati.
Alisema kuwa miradi mingi imekwama kwa sababu wanakandarasi hawawezi kuendelea na kazi bila mkataba wao kuheshimiwa.
“Wanakandarasi hata sasa wameogopa kuendesha miradi ya kaunti kwa sababu wanaadhibiwa na benki wakikosa kulipa mikopo waliyoichukua kwa wakati,” akasema Gavana Kilonzo Jnr.
Gavana wa Kirinyaga Anne Waiguru kwa upande wake alisema kuwa mgao wa Novemba aliutumia kulipa mishahara ya Novemba na kulipa ile ya Desemba pamoja na kulipa madeni waliyokuwa wakidaiwa kidharura.
“Tumeathirika kwa sababu kuna basari ambazo tunastahili kutoa kwa shule lakini hakuna pesa. Natumai kuwa pesa hizo za Desemba zitatolewa ndani ya wiki moja ijayo ili tuzielekeze kwa miradi ya maendeleo pia,” akasema Bi Waiguru.
Waziri wa Fedha wa Kaunti ya Homa Bay Solomon Obiero alisema wamelazimika kutumia mapato ya kaunti kuhakikisha shughuli zinaendelea kama kawaida.
“Tulilipa mishahara wa Desemba lakini sasa hakuna pesa za maendeleo. Tunatarajia serikali itatoa pesa hizo wiki hii,” akasema Bw Obiero ambaye anafanya kazi katika utawala wa Gavana Gladys Wanga.
Rais William Ruto alipochukua usukani alikuwa ameahidi kwamba atakomesha mtindo ambapo kaunti zimekuwa zikipokea pesa kwa kuchelewa.
Mtindo huo ulishuhudiwa sana katika enzi za utawala wa Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta.
Magavana wamekuwa wakilalamika kwamba kaunti kukosa kupokea pesa kwa wakati kumesababisha wakumbatie mikopo ghali kwenye benki.