Jamvi La Siasa

Mrengo wa G8 yaibuka vita vya ubabe vikiendelea kukikumba ODM

Na RUTH MBULA January 25th, 2026 Kusoma ni dakika: 3

MGAWANYIKO ndani ya chama cha Orange Democratic Movement (ODM), imeendelea kupanuka baada ya mrengo unaojiita G8 kumshutumu kiongozi wa chama hicho Oburu Oginga kwa hatua zinazochochea migawanyiko.

Kundi hilo, linaloongozwa na Waziri wa Ushirika Wycliffe Oparanya na kujumuisha wabunge kutoka eneo la Magharibi mwa Kenya, lilikosoa mrengo unaoongozwa na Dkt Oginga kwa kile walichokitaja kuwa ni kuweka mbele tamaa na maslahi ya kibinafsi.

Bw Oparanya alisema kuwa ingawa bado ni mwanachama mwaminifu wa ODM, anasikitishwa na yanayoendelea ndani ya chama ambayo yamesababisha mgawanyiko.

Akizungumza Shinyalu, Kaunti ya Kakamega, wakati wa hafla ya kutoa fedha za hazina za Uwezo na Hasla Ijumaa, Waziri Oparanya alieleza mshangao na huzuni yake kuhusu mienendo ya viongozi ambao wangepaswa kulinda urithi wa marehemu Raila Odinga.

Viongozi hao walielekeza lawama zao kwa Dkt Oginga na naibu wake Simba Arati, kufuatia kauli zao katika mkutano wa wajumbe wa ODM Kaunti ya Kakamega, ambako walimshutumu Bw Oparanya kwa kuchochea migawanyiko ndani ya tawi la ODM Kakamega kwa kuandaa mkutano sambamba Butere wiki iliyopita.

Dkt Oginga aliandamana na Mwenyekiti wa ODM Gladys Wanga pamoja na magavana kadhaa, akiwemo Paul Otuoma (Busia) na Fernandes Barasa (Kakamega).

“Tamaa ya pesa imeharibu viongozi. Kiongozi anazunguka huku na kule akizungumza mambo tofauti; kichwa chake kimechanganyikiwa.

Unachoshuhudia sasa hakikuwepo wakati Odinga alikuwa hai. Alikuwa mtu mwenye msimamo thabiti, ambao hangeubadilisha bila mashauriano mapana,” alisema Bw Oparanya, ambaye pia ni gavana wa zamani wa Kakamega.

Bw Oparanya aliongeza kuwa alipata wadhifa wa uwaziri kwa kupendekezwa na marehemu Raila, ambaye aliamua ODM ishirikiane na Rais William Ruto kwa manufaa ya taifa.

Walio katika mrengo wa G8 ni pamoja na Bw Oparanya, Mwakilishi wa Wanawake Kakamega Elsie Muhanda, na wabunge Nabii Nabwera (Lugari), Fred Ikana (Shinyalu), Emanuel Wangwe (Navakholo), Titus Khamala (Lurambi), Benard Shinali (Ikolomani) na Christopher Aseka (Khwisero).

Viongozi hao waliwataka viongozi wakuu wa ODM kumheshimu Bw Oparanya, wakitishia kuunda kundi jingine iwapo kiongozi wa chama Dkt Oginga hatatatua mzozo unaotikisa tawi la ODM Kakamega.

Haya yanajiri huku Mbunge wa Lugari Nabii Nabwera akisisitiza kuwa yeye ndiye mwenyekiti halali wa ODM Kakamega, wala si Gavana Barasa.

“Ninataka kumwambia Oburu Oginga mambo matatu: tulikuwa waaminifu sana kwa Raila Odinga; naye aliheshimu uaminifu wetu. Lakini uaminifu wetu hauhamishiki; mtu lazima aufanyie kazi. Oburu, unaweza kumwambia Simba Arati kwamba akimnyoshea Oparanya kidole, anatuambia tuache chama chetu? Huwezi kumtukana baba akiwa nyumbani kwake,” alisema Nabwera.

Walieleza hasira zao kuhusu kauli zilizotolewa na viongozi wa ODM katika mkutano wa wajumbe wiki iliyopita Kakamega, wakisisitiza umuhimu wa heshima.

Pia waliapa kuunga mkono Rais Ruto katika uchaguzi wa 2027 na wakataka Bw Oparanya apewe nafasi ya naibu rais, kwa kuzingatia nguvu ya kura za eneo la Magharibi.

“Usije Kakamega kumtukana Bw Oparanya. Nakupa onyo, Simba Arati. Ukimtukana Oparanya, umewatukana watu wa Kakamega,” alionya Mwakilishi wa Wanawake Kakamega Elsie Muhanda.

Aliongeza, “Kama unajua utakuja hapa kumtukana Oparanya, heri ubaki eneo lako kwa sababu kuna matatizo mengi huko. Yashughulikie; mshughulikie Matiang’i. Hukupata hata kiti kimoja cha MCA katika chaguzi ndogo za hivi karibuni. Kaa huko ufanye kazi yako.”

Akizungumza Butere, Dkt Oginga alikiri kuwepo kwa mkanganyiko kuhusu mikutano miwili sambamba ya ODM Kakamega, akisema alikuwa amealikwa kwa mikutano ya kiamsha kinywa na chakula cha mchana, lakini alikuta makundi ya wajumbe kutoka kambi tofauti yakidai kutambuliwa rasmi na chama.

“Nataka kukuuliza, ndugu yangu Oparanya, wewe ni waziri. Tunamuomba Rais William Ruto, huyu ni mbwa wako. Huyu ni mbwa wako tuliyekupa. Alikuwa miongoni mwa mbwa wetu wakuu. Lazima aambiwe afanye Kakamega kuwa bora pamoja na Gavana Barasa,” alionya Bw Arati, akimtaka Rais Ruto amkanye Oparanya na kumshutumu waziwazi kwa kuchochea migawanyiko ndani ya chama badala ya kuimarisha umoja.

Bw Arati alidai kuwa migogoro ya ndani inadhoofisha ODM katika kipindi nyeti, na akamtaka Waziri huyo kushirikiana na uongozi wa chama katika kaunti badala ya kukidhoofisha.